Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa mkopo wa Dola za Marekani
Milioni 51 sawa na takribani Shilingi Bilioni 110 kwa ajili ya kujenga
barabara ya Chaya - Nyahua Mkoani Tabora yenye urefu wa kilometa 85
ambayo itaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mkoa wa Singida na
Tabora.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa shukrani hizo jana tarehe 05 Juni, 2017 Ikulu
Jijini Dar es Salaam alipofanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa
nchini Mhe. Jasem Ibrahim Al Najem na kupokea msaada wa magari mawili ya
kusombea taka ngumu yenye thamani ya Dola za Marekani 200,000/-
yaliyotolewa na Serikali ya Kuwait kwa lengo la kuunga mkono kampeni ya
usafi hapa nchini.
“Naomba
unifikishie salamu zangu kwa Mfalme wa Kuwait, mwambie tunathamini
mchango mkubwa wa Kuwait katika maendeleo ya nchi yetu, hizi fedha za
barabara mlizotupatia zitatusaidia kumalizia sehemu hiyo ya barabara
ambayo ndio ilikuwa imebaki” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli pia aliishukuru Serikali ya Kuwait kwa kuunga mkono
juhudi mbalimbali za utoaji wa huduma za kijamii hapa nchini ikiwemo
msaada wa Dola za Marekani 250,000 kwa ajili ya kununulia vifaa katika
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na visima vya maji safi 27
vilivyochimbwa Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya wananfunzi na wananchi
wa maeneo jirani na shule.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya Kuwait kwa kutoa Dola za
Marekani Milioni 50 kwa ajili ya kuikarabati hospitali ya rufaa ya Mnazi
Mmoja iliyopo Zanzibar.
Mhe.
Rais Magufuli pia aliiomba Serikali ya Kuwait kuweka alama ya
kumbukumbu ya uhusiano wake na Tanzania kwa kusaidia ujenzi wa barabara
za Makao Makuu ya nchi Mjini Dodoma na amemhakikishia Mfalme wa Kuwait
Sheik Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania
na Kuwait hususani katika masuala ya kiuchumi ikiwemo mafuta na gesi
ambayo imevumbuliwa kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.
Kwa
upande wake Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Ibrahim Al- Najem
alielezea kufurahishwa kwake na uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya
nchi yake na Tanzania na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa Kuwait
ipo tayari wakati wowote kuunga mkono juhudi za maendeleo kulingana na
vipaumbele vya Tanzania.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye ni Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kongo Mhe. Leonard She Okitundu na
kumhakikishia kuwa Tanzania inaunga mkono juhudi za kumaliza tofauti
kati ya pande zinazopinga nchini Kongo.
Pamoja
na kukabidhi barua yenye ujumbe wa Rais wa DRC Mhe. Joseph Kabila
Kabange, Balozi Leonard She Okitundu alimueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa
hali ya Kongo ni shwari na kwamba mchakato wa mazungumzo kati ya pande
zinazopingana nchini humo unaendelea vizuri.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli alifanya mazungumzo na Mjumbe Maalum
wa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji ambaye ni Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo
Jenerali Atanasio Salvador Ntumuke.
Baada
ya mazungumzo hayo, Jenerali Atanasio Salvador Ntumuke alisema Msumbiji
itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa mambo mbalimbali kwa kuwa nchi
hizo ni ndugu na zimesaidiana kwa mengi tangu harakati za kupigania
uhuru ambapo Tanzania ilitoa mchango mkubwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments:
Chapisha Maoni