Sekta
ya madini imekua kwa asilimia 17.5 ikilinganishwa na asilimia 11.5 ya
mwaka 2016 ambapo ongezeko hilo limetokana na kuimarishwa kwa udhibiti
wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini, kuimarishwa kwa ukaguzi na
usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini pamoja na
usafirishaji wa madini nje ya nchi.
Waziri
wa Madini,Angellah Kairuki amesema hayo jana,Mei 31, 2018 Bungeni
Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na
matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Ukuaji
wa sekta ya madini pia kumetokana na kuongezeka kwa viwango vya mrabaha
na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya
sheria ya madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 na kanuni zake,”
alisema Angellah Kairuki.
Aidha
alisema, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea
kuimarika ambapo katika mwaka 2017 mchango huo ulifikia asilimoa 4.8.
Kwa upande wa thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi, mauzo yalifikia
Dola za Marekani 1,810,697,000 mwaka 2017.
“Ni
matarajio yetu kuwa thamani ya mauzo inaendelea kuongezeka tena baada
ya kukamilisha mageuzi makubwa ambayo tuliyaanzisha ikiwa ni pamoja na
uongezaji thamani madini ndani ya chini,” alisema Mhe. Kairuki.
Waziri
Kairuki alizitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa Fedha
2018/2019 na Wizara ya Madini na Taasisi zake kuwa ni pamoja na
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali
madini, kuwaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na
kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini.
Alizitaja
kazi nyingine kuwa ni kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama,
afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na
mikubwa, kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya
Sekta ya Madini, kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi
kufaidika na rasilimali madini, kuelimisha Umma na kuboresha mawasiliano
kati ya Wizara na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini.
Wizara
ya Madini imeomba kuidhinishiwa na Bunge jumla ya shilingi
58,908,481,992 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka
wa Fedha 2018/2019.
0 comments:
Chapisha Maoni