Kada
wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Abdallah Safari amemfagilia Rais
Magufuli kwa kupigania rasimali za taifa ikiwemo madini yaliyokuwa
yakiwanufaisha Wawekezaji.
Akizungumzia
hatua ya Rais Magufuli kuitisha tume mbili za uchunguzi wa Mchanga wa
Madini na kubaini madudu kwenye uwekezaji katika sekta ya Madini ikiwemo
baadhi ya kampuni kutosajiliwa ikiwemo kampuni ya ACACIA, Prof Safari
amesema kutokana na juhudi binafsi anazofanya kutetea rasilimali za nchi
anamfananisha Magufuli na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah na
Waziri Mkuu wa Kwanza wa Congo (DRC), Patrice Lumumba
Licha
ya Prof.Safari mwingine aliyempongeza Rais Magufuli ni Mbunge wa
Chambani, Yusuf Salim Hussein (CUF) ambaye amesema anamuunga mkono Rais
Magufuli, kwani amejitoa mhanga kwa maslahi ya taifa.
Aliongeza kuwa vita hiyo ni ngumu na wanapaswa kumshukuru Rais bila ya kujali kama ni wa CCM, Chadema au CUF.
“Ninampongeza
Rais John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kutetea rasilimali za
nchi. Anafanya kazi kama walivyokuwa wanafanya baadhi ya viongozi
wazalendo barani Afrika ya kupigania haki za wananchi wao kufaidika na
rasilimali za nchi,” alisema Profesa.
Alitoa
mfano wa Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah na Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere kama viongozi waliojitolea kwa ajili ya wananchi wao.
Alisema
maamuzi anayoyafanya Rais yanasimama katika Kifungu cha Tisa (Kifungu
Kidogo C) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na
marekebisho ya mwaka 2000, ambacho kinasisitiza kwamba utajiri wa Taifa
uendelezwe, uhifadhiwe na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa
jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.
Profesa
Safari aliwaomba Watanzania na wataalamu wa sheria za mikataba, kuunga
mkono juhudi zinazofanywa na Rais katika kutetea maslahi ya Taifa.
“Nchi
hii ina wanasheria wengi wazuri katika masuala ya madini na mikataba.
Ninashauri watafutwe wataalamu hawa watakaokuwa sio wala rushwa ili
wamsaidie Rais katika vita hii ya rasilimali,” aliongeza Profesa Safari.
Juzi
Rais Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya Pili ya Madini ya kuangalia
masuala ya kisheria na kiuchumi, ambapo ilionesha Serikali imekuwa
ikipoteza mapato ya Sh trilioni 108.46 kutokana na udanganyifu,
unaofanywa katika usafirishaji wa mchanga wa dhahabu ‘makinikia’ nje ya
nchi katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi mwezi Machi 2017.
Wakati
huo huo, Bunge linatarajiwa kutoa Azimio la kumuunga mkono Rais
Magufuli kutokana na kazi nzuri, zilizofanywa na kamati mbili
alizoziteua kuchunguza mchanga wa dhahabu (makinikia) zilizobaini wizi
mkubwa, anaripoti Mgaya Kingoba kutoka Dodoma.
Wabunge
wengi wakiwamo wa Kambi ya Upinzani, walisema jana kuwa wameikubali
kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli katika suala la madini, ingawa
wao walinyoosha kidole kwa Serikali ya CCM kuwa ilishindwa kuzuia wizi
huo.
Wabunge
wote waliochangia jana walitoa pongezi kwa Rais Magufuli kutokana na
kazi nzuri ya kamati zake mbili; ya kwanza ya wataalamu wa jiolojia na
kemia na ya pili ya wachumi na wanasheria, ambazo zimeibua wizi mkubwa
uliofanywa na kampuni za uchimbaji madini.
0 comments:
Chapisha Maoni