test

Jumanne, 18 Oktoba 2016

Tanzania yakana kujitoa kwenye mchakato wa Viza ya pamoja EAC


Serikali ya Tanzania imekanusha kugomea suala la uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kuongeza kwamba Viza hiyo ya pamoja bado haijaanzishwa rasmi.

 



Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta ya Uzalishaji, Bw. Bernard Haule

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta ya Uzalishaji, Bw. Bernard Haule imeeleza kuwa, Tanzania inashiriki kikamilifu katika mchakato wa uanzishwaji wa Viza hiyo.



Bw. Haule amesema, kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa EAC, baada ya mkutano wa tano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori, lililokaa Julai mwaka 2013, Jijini Bujumbura nchini Burundi ambapo nchi wanachama walikubaliana kuundwa kwa kikosi kikazi kitakachoangalia namna viza hiyo itakavyonufaisha nchi wanachama na uendeshwaji wake hasa kiusalama.

Bw. Haule amesema Tanzania inatambua umuhimu wa Viza ya pamoja ya utalii na kwamba inasubiri kuanzishwa kakwe kwa hamu kubwa kutokana na manufaa yake lakini ni vyema kwanza mapendekeo na masuala muhimu yazingatiwe kama vile kuanzishwa sheria viza za nchini wanachama, Idara ya Uhamiaji kuanzia mfumo wa kudhibiti usalama na utoaji wa Viza kwa mfumo wa kielektroniki.

Mengine ni kuwepo kwa ukusanyaji na ugawaji wa mapato pamoja na namna ya kulipa, kuwepo kwa maafisa uhamiaji katika kila ofisi za balozi pamoja na kuwajengea uwezo watumishi kwenye suala la mfumo wa utoaji Viza ya pamoja ya utalii.

Chanzo: EATV

========
TAMKO:


Screen Shot 2016-10-18 at 17.52.39.png 

Ndugu wanahabari:

Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii ya hapa nchini na nje ya nchi iliandika taarifa kuhusu Tanzania kujitoa au kugomea utaratibu wa visa ya pamoja ya utalii (Single Tourist Visa) wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Kufuatia taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa ikipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari kutaka kufahamu ukweli wa jambo hilo. Hivyo, Wizara imeona leo itoe taarifa rasmi kufafanua namna ya mchakato wa uanzishwaji wa viza ya pamoja ya utalii ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unavyoendelea.

Suala la Uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki bado liko katika majadiliano ya Nchi Wanachama kupitia Vikao vya Sekta ya Utalii na Wanyamapori. Katika kufanikisha azma hii, Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Maliasili na Usimamizi wa Wanyamapori uliofanyika tarehe 1 Novemba 2008 liliunda Kikosi Kazi kwa ajili ya kufanya utafiti kwa lengo la kubainisha mahitaji na utayari wa Nchi wanachama juu ya kuanzisha Viza ya Pamoja ya Utalii. Utafiti uliofanyika mwaka 2010, ulibainisha masuala muhimu yafuatayo ya kuzingatiwa kabla ya kuanzishwa kwa Viza ya Pamoja ya Utalii:

a) Kurazinisha (harmonization) sheria za Viza za Nchi Wanachama;

b) Idara ya Uhamiaji kuanzisha Mfumo wa kudhibiti Usalama;

c) Utoaji wa Viza kuwa wa kielektroniki;

d) Kuwepo kwa mfumo wa ukusanyaji na ugawanyaji wa mapato pamoja na namna ya kulipa;

e) Kuwepo kwa maafisa uhamiaji katika kila ofisi za ubalozi;

f) Kujenga uwezo wa watumishi kwenye suala la mfumo wa kieletroniki wa utoaji wa viza ya pamoja ya Utalii.

Kufuatia matokeo ya utafiti huo, Mkutano wa 5 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori uliofanyika mwezi Julai 2013 jijini Bujumbura, Burundi pamoja na mambo mengine uliagiza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kitajumuisha wataalamu kutoka Taasisi za Uhamiaji, Utalii, Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tehama, Usalama, na Sheria katika nchi wanachama ili kuandaa mpango kazi na kushughulikia masuala yote ambayo yatajitokeza kuhusiana na uanzishwaji wa Viza ya Pamoja ya Utalii. Hata hivyo, kabla ya utekelezaji wa maagizo hayo, Nchi za Uganda, Kenya na Rwanda zilianzisha Viza ya Pamoja ya Utalii baina yao nje ya vikao vya Jumuiya.

Ni vema ikaeleweka kwa umma wa Watanzania na Afrika Mashariki kwa Ujumla kuwa kwa kuzingatia Mfumo wa Maamuzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao ni wa kukubaliana kwa pamoja (consensus) hakuna Mfumo wowote wa uanzishwaji wa Visa ya Pamoja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioanzishwa. Hii inamaanisha kuwa hakuna Visa ya Pamoja ya Utalii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokubalika. Kwa mantiki hiyo, taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari hazina ukweli wowote na zilikuwa na lengo la kuichafua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawawahakikishia umma wa Tanzania kuwa itaendelea kuheshimu maamuzi ya vikao halali vya Jumuiya na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha visa ya pamoja ya utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 



Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 18 Oktoba 2016.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx