
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers
Siang’a amesema kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya walitaka kumuua
wiki iliyopita.
Kamishna
Siang’a ameeleza hayo katika mahojiano maalum aliyofanya na gazeti la
Mwananchi kuhusu maendeleo ya vita dhidi ya biashara hiyo haramu, ikiwa
ni takribani miezi mitano tangu ateuliwa kuongoza kitengo hicho nyeti.
“Wiki
iliyopita tu hapa [wauza dawa za kulevya] walitaka kuniua,” alisema
Siang’a ingawa hakueleza kwa kina kuhusu jaribio hilo baya dhidi yake.
“Wanaofanya biashara hii wana uwezo wa kufanya chochote wanachotaka.
Kabla jamii haijatuhukumu ni vyema ikatambua kuwa tuna changamoto
kubwa,” aliongeza.
Katika
hatua nyingine, Kamishna Siang’a alisema kuwa wanaofanya biashara hii
haramu ni watu wakubwa ambao hufadhili kazi za Serikali, viongozi
wanaowalina na madhehebu mbalimbali ya dini.
Alisema
kuwa yupo mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya ambaye alikuwa
akionekana kama mtu mwema sana kwenye jamii, akifadhili taasisi moja ya
Serikali pamoja na kuwasomesha watoto wa vigogo na kufadhili shughuli
zao za harusi, lakini ameshakamatwa na anatumikia kifungo cha maisha
jela.
Hata
hivyo, Siang’a alisema kuwa wamepata taarifa kuwa mfanyabiashara huyo
anaishi maisha ya kifalme gerezani na kwamba huenda hata usiku halali
ndani ya gereza hilo.
“Tunapata
taarifa kuwa anahudumiwa vizuri gerezani, na inavyosemekana kuwa huenda
halali hata huko. Anachukuliwa usiku na kupelekwa kwake kulala, asubuhi
anarudishwa,” alisema.
Alitoa
mfano mwingine wa nguli wa dawa za kulevya aliyefungwa gerezani, kuwa
kabla ya kuingia alikarabati gereza na kukodisha nyumba za jirani kwa
ajili ya kuweka watu ambao watakuwa wanampikia vyakula, hivyo ameendelea
kuwa na afya nzuri akiwa gerezani.
Alisema hayo yote hufanyika kwa ushirikiano wa baadhi ya askari wa gerezani na wakuu wa gereza husika.
Kamishna
Siang’a alisema kuwa Mamlaka hiyo hairudishwi nyuma na kwamba hadi sasa
wameshawakamata vinara 15 wa dawa za kulevya ambao amewataja kama watu
wenye jeuri ya pesa.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:
Chapisha Maoni