Kampuni
ya uchimbaji madini ya Acacia, imesema kuwa inafanya kazi nchini kwa
misingi ya sheria na Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA)
inatambua uwepo wake.
Kauli
hiyo imekuja baada ya juzi taarifa ya pili ya wachumi na wanasheria
iliyofanya uchunguzi wa mchanga wa madini katika makontena yalizuiwa
kusafirishwa kwenda nje ya nchi, kubainisha kuwa kampuni hiyo haina
kibali na inafanya kazi kinyume na sheria.
Taarifa
iliyotolewa na kampuni hiyo jana pia imesema kuwa Acacia itafanya
mkutano na wanahisa wake kesho kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sakata zima.
Kampuni hiyo ilieleza kuwa migodi yake ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara inaendeshwa kisheria.
“Acacia inapenda kuthibitisha kwamba inaendelea kufanya kazi katika migodi yake mitatu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.
“Migodi
hii yote inamilikiwa na kuendeshwa na makampuni ambayo yamesajiliwa
Tanzania kisheria; Bulyanhulu Gold Mine Limited, Pangea Minerals Limited
na North Mara Gold Mine Limited ambayo yana leseni maalumu kwa kila
mgodi,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Acacia ambayo tumeiweka hapo
chini.
Taarifa
hiyo iliendelea kueleza: “Kampuni hizi zinamilikiwa na Acacia ambayo
imesajiliwa nchini Uingereza ingawa umiliki huu si wa moja kwa moja
(indirectly owned).
“Muundo
huu ni wa uwazi, upo kisheria na huwekwa wazi katika taarifa zetu za
hesabu za mwaka ambazo hukaguliwa kwa mujibu wa taratibu za kimataifa.”
Taarifa
hiyo iliendelea kufafanua kwamba utaratibu huo wa umiliki uliwekwa wazi
kwa CMA wakati Acacia ikijioredhesha katika Soko la Hisa la Dar es
Salaam (DSE) mwaka 2011.
“Muundo
huu ni sehemu ya taarifa ambayo ilipitishwa na CMSA kwa ajili ya
kujiorodhesha DSE. Tangu kujisajili DSE kilichobadilishwa ni jina la
Acacia kutoka African Barrick Gold Plc kuwa Acacia Mining Plc,” inasema
taarifa hiyo.
Katika
hatua nyingine, Acacia wametangaza kufanya mkutano na wanahisa wake kwa
mtandao kesho kutoa ufafanuzi zaidi juu ya sakata zima.
Walipofuatwa
DSE kutoa maelezo ni kwa vipi kampuni ambayo haina usajili kuweza
kujiorodhesha na kuuza hisa, walisema wao si wasemaji kwa kuwa mchakato
wa kujiorodhesha huongozwa na kusimamiwa na CMSA na hivyo kumshauri
mwandishi awasiliane nao.
Mwandishi
alipowasiliana na Ofisa Habari wa CMSA, Charles Shirima, alisema mtu
aliyekuwa akishughulikia suala hilo alikuwa safarini Dodoma na kumtaka
mwandishi awasiliane naye leo.
0 comments:
Chapisha Maoni