Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia walimu wawili
na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chang'ombe (Mazoezi) kwa tuhuma za
kukutwa na mtihani wa Kemia wa kidato cha sita. Mitihani hiyo inaendelea
kufanyika nchini.
Kamishna
wa Kanda hiyo, Simon Sirro, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Musa Elius
na Innocent Murutu ambao ni walimu wa shule hiyo. Mwanafunzi ni Ritha
Mosha.
Kamishna
Sirro alisema wiki iliyopita saa 1:00 usiku Jeshi la Polisi lilipokea
taarifa kutoka kwa Ofisa wa Baraza la Mitihani, Aron Mweteni, aliyesema
alimkuta kwenye shule hiyo mwalimu Elius na mtahiniwa Ritha wakiwa na
karatasi yenye maswali na majibu ya somo la vitendo la kemia.
Alisema
baada ya kuwatilia shaka na baadaye kuwatia mbaroni, walifanya
ufuatiliaji wa awali kwa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) ambako
ilibainika kuwa mtihani huo ni miongoni mwa ile ya kidato cha sita
inayofanyika mwaka huu.
"Watuhumiwa
wanaendelea kuhojiwa polisi na upelelezi ukikamilika tutawachukulia
hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani," Sirro alisema.
Katika
tukio lingine, Kamishna Sirro alisema mvua zinazoendelea kunyesha
jijini Dar es Salaam zimesababisha kifo cha mkazi wa Gulani Suka, Alice
Genadi ambaye alitumbukia kwenye shimo la choo cha jirani yake ambacho
kilikuwa kimejaa maji na hakikuwa kimefunikwa.
Kamanda Sirro alisema msichana huyo alikuwa akimfuata dada yake dukani.
Wakati huo huo, Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kukutwa na vipande sita vya meno ya tembo.
Pia
kamanda Sirro alisema wanawashikilia watuhumiwa watatu waliodaiwa
kukutwa na lita 36,000 za gongo yenye thamani ya Sh. milioni 72.