Mshtakiwa
anayekabiliwa na kesi ya kujaribu kubaka Allen Robert (33), ametoroka
akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza baada ya kutoka kusikiliza
ushahidi wa kesi inayomkabili na kusababisha taharuki kwa baadhi ya
wananchi waliokuwa eneo hilo.
Tukio
hilo lilitokea jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni jijini
Dar saa tisa alasiri na askari Magereza walilazimika kurusha risasi
hewani ili kumkamata.
Wananchi waliohudhuria mahakamani kwa shughuli mbalimbali baadhi walikimbia baada ya kusikia milio ya risasi.
Mmoja
wa wananchi waliokuwa eneo hilo, Alex Simon alisema baada ya kusikia
milio ya risasi aliingia chini ya meza na alilala chini akihofia usalama
wake.
“Wakati
nikiwa nimeagiza chakula kwenye mgahawa ghafla niliona mtu akitoka
hapo kwenye geti la Mahakama kisha nikasikia sauti ya askari Magereza
wakisema lala chini wakati huo yule mshtakiwa akikimbia katikati ya
watu. Nililala chini ya meza baada ya dakika 15 hali ilikuwa shwari,” alisema Simon.
Baada
ya Robert kukamatwa alifunguliwa shtaka na kupandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Mwanzo Kinondoni kwa kutoroka akiwa chini ya ulinzi.
Mbele
ya Hakimu Marko Mochiwa, Mwendesha mashtaka wa Polisi, Mrusha Warioba
alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 10 katika viwanja vya Mahakama
ya Wilaya ya Kinondoni.
“Mshtakiwa
unakabiliwa na shtaka la kumtoroka askari Magereza Koplo John Chale,
ulifanya hivyo ukijua kwamba ni kinyume na sheria,” alidai Warioba.
Baada ya maelezo hayo mshtakiwa hakujibu chochote licha ya kuulizwa zaidi ya mara mbili.
Hakimu Mochiwa aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 16 kesi hiyo itakaposikiliza. Mshtakiwa alipelekwa rumande.
Katika
kesi ya msingi iliyopo mbele ya Hakimu Issa Kasailo, mshtakiwa
anakabiliwa na shtaka la kujaribu kumbaka binti mwenye umri wa miaka
24.
Kesi hiyo ilitajwa mahakamani hapo jana kwa ajili ya kuendelea na ushahidi na shauri liliahirishwa hadi Mei 24.