Mbunge
wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM), amewapiga mkwara mawaziri bungeni
kuwa atahamasisha wananchi wa jimbo lake kwenda kuzima mtambo wa maji
ulioko Ziwa Victoria.
Kitwanga
ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa kwanza katika serikali ya
awamu ya tano, alilieleza Bunge jana kuwa mtambo huo upo kwenye chanzo
cha maji cha Iherere, kilichoko jimboni kwake Misungwi mkoani Mwanza.
Katika
mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji bungeni
mjini Dodoma jana mchana, mbunge huyo aliyekuwa wa kwanza kupewa nafasi
ya kuchangia, alitoa onyo hilo kwa Waziri Gerson Lwenge na msaidizi
wake, Mhandisi Isack Kamwele, kwamba yuko mbioni kuuzima mtambo huo
ikiwa wananchi wake hawatakuwa sehemu ya mradi huo wa maji.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, jimboni kwangu hakuna maji ya uhakika na tangu mwaka 2008
wananchi wamekuwa wakiyasubiri bila mafanikio," Kitwanga alisema.
“Kwa
hiyo, nitakachokifanya safari hii, sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali
nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende
tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose.
“Wanamchi
wa Misungwi hawana maji na katika bajeti yenu leo (jana) mmesema
Nyang’omango kuna maji wakati hakuna, sasa nawaambia, sitatoa shilingi
'nita-mobilize' (nitahamasisha) wananchi tukazime ule mtambo.
“World
Bank' (Benki ya Dunia) walifika pale kijijini, wakasema hawa wananchi
walioko kwenye kile chanzo wanatakiwa kupata maji, lakini nyie hamuoni,
hivi nyie mkoje?
“Nakipenda
chama changu (CCM), nampenda Rais wangu (John) Magufuli, lakini lazima
tutendeane haki kwa sababu hii nchi ni yetu sote.
“Hamuwezi
kupeleka maji sehemu nyingine kwa gharama ya Sh. bilioni 600 halafu
mkashindwa kuwapa wananchi wangu hata mradi wa Sh. bilioni 10.
“Mshukuru
kwamba nilipokuwa waziri, nilikuwa siwezi kusema kitu, lakini sasa
nimetoka, tutapambana kwa sababu lazima tuwe na mipango mizuri ya
kuwapelekea wananchi wetu maji kama inavyofanyika katika umeme kupitia
REA (Wakala wa Umeme Vijijini).”
Kitwanga
alitumbuliwa na Rais Magufuli Mei 20, mwaka jana kwa tuhuma za kuingia
bungeni na kujibu swali linalohusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
akiwa amelewa.
Kitwanga
pia alilalamikia kile alichokiita tabia ya baadhi ya viongozi wa wizara
hiyo kukwamisha upatikanaji wa maji kupitia kwa marafiki zake kutoka
nchini Austria.
“Rais
alipokuja Misungwi, aliwaambia wananchi, kwamba nina marafiki zangu
huko nje wanaoweza kunisaidia kupata maji," alisema. "Ule mradi
ulipokuja, nikawekewa figisu wakasema mimi nina 'interest' (maslahi)
nao.
"Ni kweli nina 'interest' nao kwa sababu wananchi wangu wa Kolomije wanahitaji maji, wananchi wa Bukumbi wanahitaji maji.
“Kwa
hiyo, Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena, safari hii sitatoa
shilingi, nitakwenda kuwahamasisha wananchi wangu tukazime ule mtambo wa
maji ili wote tukose,” alisisiza Kitwanga.
Hata
hivyo, muda mfupi kabla ya kusitisha shughuli za Bunge jana mchana,
Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alimtahadharisha Kitwanga kuwa,
uamuzi wake huo huenda ukamsababishia matatizo kwa kuwa unakiuka sheria
za nchi.
Dk.
Tulia alisema kuwahamasisha wananchi ili wavunje sheria ni kosa la
jinai, hivyo mbunge huyo anapaswa kuwa makini kwa kuwa anaweza
kuchukuliwa hatua kabla hata hajawahamasisha wananchi wa maeneo ya
Kolomije na jimbo zima la Misungwi.