Na mwandishi wetu, Arusha
Wadau
wa sekta ya mifugo mkoani Arusha wameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) kuwasaidia katika kuendeleza sekta hiyo kwa kuwapatia
mikopo na mahitaji mengine kwa ajili ya kuongeza tija katika ufugaji wa
kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa.
Akizungumza
katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Kampuni ya Nyama ya
Arusha, kwa niaba ya wafugaji wa mkoa wa Arusha, Kaimu Meneja wa Kiwanda
cha Nyama cha Arusha, Bw. Fabian Kissiagi amesema ukosefu na ufinyu
mkubwa wa upatikanaji wa fedha za mtaji kwa ajili ya maendeleo ya kilimo
hasa katika sekta ya mifugo inawapa changamoto katika uendelezaji wa
sekta ya mifugo nchini.
Bw.
Kissiagi ameongeza ukosefu wa mikopo ya uhakika inarudisha nyuma ukuaji
wa sekta ya mifugo na kurudisha nyuma juhudi za serikali katika
kuendeleza sekta ya mifugo.
“Hali
ya ukosefu wa mitaji ya uhakika inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mikopo
mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara
za bidhaa na kutusahau sisi wakulima na wafugaji, hivyo tunaiomba TADB
kutusaidia kutatua changamoto hii,” alisema.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
amesema Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania
(TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini kote
ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza
mapinduzi katika kilimo nchini.
Bw.
Assenga ameongeza kuwa sekta ya mifugo ni mojawapo ya minyororo ya
mwanzo inayopatiwa mikopo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao na
mifugo mbalimbali hasa katika uongezaji wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe
wa nyama na maziwa nchini.
Ameongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa.
“Benki
inatoa mikopo na kusaidia uwekezaji kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa
mitambo na ufungaji wa mitambo ya kuhudumia ng’ombe ikiwemo majosho na
mabwawa ya kunyweshea na pamoja na usindikaji wa nyama na maziwa kwa
ajili ya kuongeza thamani nyama na maziwa,” alisema Bw. Assenga.
Naye,
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha amesema
kuwa TADB inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi
(Hadi Miaka Miwili (2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi
Miaka Mitano (5)) na Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka
Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo
hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia
Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara
ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.
Mkoa
wa Arusha unashika nafasi ya tatu kati ya mikoa yenye mifugo mingi
nchini ambapo inakadiriwa kuwa na zaidi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo
milioni tatu.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (aliyesimama)
akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa Mifugo
mkoani Arusha kuhusu fursa za mikopo ya TADB. Kikao hicho kilifanyika
katika Kampuni ya Nyama ya Arusha, jijini Arusha.
Mkurugenzi
wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha (aliyesimama)
akizungumza kuhusiana na mikopo na huduma zinazotolewa na TADB katika
kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa Mifugo. Kikao hicho
kilifanyika katika Kampuni ya Nyama ya Arusha, jijini Arusha.
Kaimu
Meneja wa Kiwanda cha Nyama cha Arusha, Bw. Fabian Kissiagi
(aliyesimama) akizungumzia changamoto zinazoikabilia sekta ya mifugo
mkoani humo katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Wadau wa Mifugo
mkoani Arusha.
Meneja
wa Uendelezaji wa Biashara wa TADB, Bw. Geofrey Mtawa (wa pili kulia
aliyesimama) akitoa takwimu za mahitaji ya mikopo ya mkoa wa Arusha.
Kulia ni Afisa Mwandamizi wa Uendelezaji wa Biashara wa TADB, Bw.
George Nyamrunda.
Baadhi
ya Wadau wa Mifugo mkoani Arusha waliohdhuria kikao cha pamoja na TADB
wakitoa maoni yao kuhusiana hali ya hupatikanaji wa mikopo katika
kusaidia sekta ya mifugo mkoani humo.
Ugeni
kutoka TADB wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wadau wa Mifugo
mkoani Arusha mara baada ya katika kikao cha pamoja kati ya TADB na
Wadau wa Mifugo. Kikao hicho kilifanyika katika Kampuni ya Nyama ya
Arusha, jijini Arusha.