Mbunge
wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), amesema wananchi wamewageuza
wabunge wa Tanzania na kuwa kama mashine za kutolea fedha (ATM) na Vyama
vya Kuweka na Kukopa (SACCOS).
Kutokana na hali hiyo, amesema kuna haja Serikali kuboresha mafao yao ili yaendane na majukumu wanayokabiliana nayo.
Waitara
aliyasema hayo jana mjini hapa wakati wa semina ya wabunge walioko
katika mabunge ya nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CPA).
“Mshahara
wa mbunge kila mwezi unakatwa shilingi milioni 1.2, lakini baada ya
kumaliza miaka mitano ya ubunge, mafao yake yanakatwa tena.
“Hivi
huo utaratibu mliutoa wapi wakati haupo nchi yoyote duniani? Sisi
wabunge tumegeuzwa kama ATM au saccos kwa sababu tutatoa pesa kila
mahali.
“Kule
Kenya ofisi ya mbunge ni kama taasisi kwa sababu ina mbunge na ina
mtafiti anayemsaidia mbunge kila anapotaka kufanya mambo yake.
"Hata
kukiwa na harambee, mbunge unaitwa na kutakiwa uchangie fedha nyingi,
sasa utachanga kwa fedha zipi wakati mnatulipa kidogo, yaani huu ni
mzigo kwetu wabunge.
“Kwa hiyo, tuongezeeni mafao kwa sababu tunalipwa kidogo sana ikilinganishwa na nchi zingine,”alisema Waitara.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM), pamoja na
kulalamikia mafao madogo, alitaka kujua takwimu halisi za malipo
wanayolipwa wabunge wa Kenya na nchi zingine ili wayalinganishe na
wanayolipwa wabunge wa Tanzania.
Naye
Mbunge wa Viti Maalum, Shally Raymond (CCM), alisema kuna haja kwa
wabunge hao kuboreshewa mafao yao ili waweze kufanya kazi kwa mafanikio
zaidi.
Mbunge
wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), pamoja na kulalamikia mafao,
alilalamikia utaratibu wa vyama vya siasa kukutanisha wabunge wao ili
wakubaliane kupitisha mambo yenye masilahi ya chama badala ya kuangalia
utaifa.
Wakati
hao wakisema hayo, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alitaka
wabunge wawekewe bima ya afya ya maisha kama sheria inavyotaka.
“Kwanza kabisa nimeshangaa kusikia makao makuu ya CPA Barani Afrika yapo Tanzania na pia ofisi yao iko hapa bungeni.
“Kuhusu
hilo suala la bima ya afya ya maisha ya wabunge, nashangaa kwanini
Serikali haitaki kuliruhusu kwa wabunge kwani hata Tume ya Utumishi ya
Bunge, imekuwa ikisisitiza juu ya jambo hilo.
“Yaani
Tume ya Utumishi imelifuatilia kwa muda mrefu, lakini Serikali haitaki
kukubali, jambo ambalo hakitendi haki kwa sababu baadhi ya wabunge
wameshafariki na wengine wamepata ulemavu,” alisema Lugola.
Hata
hivyo, wakati akijibu hoja hizo, Katibu wa Spika wa Bunge, Said Yakub,
alisema chanzo cha wabunge kugeuzwa ATM ni wao wenyewe kwa sababu ndivyo
walivyowazoesha wapiga kura wao.
0 comments:
Chapisha Maoni