Serikali
mkoani Kilimanjaro imeagiza jeshi la polisi mkoani hapa, kufanya
ukaguzi maalumu wa magari yanayobeba wanafunzi hususani shule binafsi
ili kujiridhisha kama yana sifa ya kufanya kazi hiyo.
Mkuu
wa mkoa huo, Saidi Mecki Sadiki alisema hayo wakati wa Kikao cha
Ushauri cha Mkoa (RCC) ambacho kilikuwa maalumu kwa suala la hifadhi ya
mazingira.
“Kikosi
cha usalama barabarani kiandae mpango wa ukaguzi wa magari ya wanafunzi
kila Jumamosi na yale yasiyo na sifa yaondolewe barabarani....hatuwezi
kukaa kimya huku tunaendelea kupoteza maisha ya watoto wetu kama
ilivyotokea mkoani Arusha” alisema.
Sadiki
alisema Serikali ilisikitishwa na vifo vya watu wasio na hatia kwani
pia katika ajali hiyo mkoa wake uliguswa kwa kupoteza watoto 14.
Alimtaka Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issa kusimamia
kikamilifu ukaguzi huo ili kuepuka udanganyifu.
Ajali
ya basi la shule Lucky Vicent ilitokea Mei 6, 2017 katika eneo la
Rhotia Marera, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha na kusababisha vifo vya
wanafunzi 32 pamoja na walimu wawili na dereva wa basi hilo.
Jeshi
la polisi mkoani Arusha tayari limeeleza chanzo cha ajali kuwa pamoja
na mwendo kasi, lakini pia wanafunzi na walimu hawakuwa wamefunga
mikanda jambo ambalo lingepunguza athari za ajali.
Aidha,
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema pia gari
hilo lililokuwa na uwezo wa kubeba watu 30, lilibeba 38 kinyume na uwezo
wake