Mbunge
wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, ametoa maoni yake
kuhusu ushauri wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk.
Harrison Mwakyembe aliyewataka wasanii wa Tanzania kuacha kuimba nyimbo
zenye jumbe za kisiasa kwani hawatafanikiwa.
Profesa
Jay ambaye ni rapa nguli wa kizazi kipya aliyewahi kuweka rekodi maalum
ya albam yake ya ‘Mapinduzi Halisi’ iliyokuwa na jumbe zenye mlengo wa
kisiasa na kijamii, amesema ameshangazwa na kauli ya Waziri.
“Kuwaambia
wasanii kuwa waimbe nyimbo za maisha yao tu na washindwe kuimba vitu
vingine, maana yake unataka kutoa ‘green light’ kwa wasanii sasa waanze
kuimba mambo ya mapenzi… nakupenda, nakupenda..,” alisema Profesa Jay.
“Maana
yake unaweza kuchochea kuhusu masuala ya mapenzi tu na kushindwa
kufanya vitu vya kijamii ambavyo vingeweza kulipeleka taifa letu mbele.
Mimi naamini msanii ana sauti kubwa na anaweza kupaza sauti positively
na ikasaidia taifa letu ideologically (kiitikadi), socially (kijamii),
culturally (kitamaduni), economically (kiuchumi), politically (kisiasa)
pamoja na sustainable development (maendeleo endelevu),” aliongeza.
Mbunge
huyo alidai kuwa wapo wasanii walioimba kuhusu siasa na masuala ya
kijamii kama 2Pac, BIG, Bob Marley, Lucky Dube na wengine ambao
walisaidia dunia kuhama katika ngazi moja kijamii hadi ngazi nyingine.
Hata
hivyo, Profesa Jay alikubaliana na hoja ya Waziri Mwakyembe kuwa
wasanii hawapaswi kuitukana Serikali, akieleza kuwa wanapaswa kuachwa
watoe mawazo yao mbadala ikiwa ni pamoja na kuisifia Serikali.
Akizungumza
Bungeni mjini Dodoma, Waziri Mwakyembe aliwashauri wasanii kuachana na
nyimbo za siasa kwani hawatafanikiwa kwakuwa hakuna msanii ambaye
alijikita katika kuimba siasa na akafanikiwa.