Rais
Mstaafu wa awamu ya tatu, Mzee Benjamin Mkapa amevikosoa vyombo vya
habari barani Afrika na haswa kusini mwa Jangwa la Sahari kwa kile
alichosema vingi vimejikita katika kuripoti habari za kisiasa na matukio
ya nani kafanya nini au kawa nani, badala ya kuripoti habari za uchumi
za kuwasaidia wananchi.
Mzee
Mkapa aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahijiano na na Idhaa ya
Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) ya nchini Ujerumani ambapo alisema
kwenye vyombo vya habari vya Afrika kuna upungufu mkubwa wa wa habari za
uchumi na maendeleo zilizofanyiwa utafiti wa kina.
“Tatizo
moja kubwa la vyombo vya habari vya nchi za Afrika hasa hasa Kusini mwa
Jangwa la Sahara ni kwamba habari nyingi zinazopewa kipaumbele ni zile
za kisiasa na zinazohusu nani ni nani na kafanya nini.”
“Kuna
upungufu mkubwa wa habari za kiuchumi na maendeleo zilizofanyiwa
utafiti wa kina na zinazochochea maendeleo. Kuna habari kidogo sana za
utetezi wa kimaendeleo na kujipanga ili tupige hatua.”
Kufuatia
hali hiyo, Mzee Mkapa alisema kuwa uhuru wa vyombo vya habari unaodaiwa
kuwa umebanwa, unahusu vyombo vya habari ambavyo havina mchango kwenye
maendeleo ya uchumi wetu zaidi ya kuzungumzia matokeo badala ya
uchambuzi.
“Kwa
hiyo, huo uhuru wa vyombo vya habari unaosema unabanwa unahusu kundi la
vyombo vya habari ambavyo havina mchango wowote katika uchambuzi wa
masuala ya uchumi utetezi wa maendeleo wala kwenye kujipanga kujitafutia
maendeleo. Nasi ni taifa masikini linalohitaji kuendelea. Nadhani ni
uamuzi sahihi.” alisema Mzee Mkapa.
Kauli
hii ya Mzee Mkapa ilikuja baada ya kuulizwa kuhusu madai ya kuwa
serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inabana
uhuru wa vyombo vya habari hali ambayo haikuwapo miaka ya nyuma.