Wachimbaji,
wauzaji na wasafirishaji wadogo wa madini, wamemwomba Rais Dk. John
Magufuli kuondoa zuio la kusafirisha mchanga wenye madini alilolitoa
wiki iliyopita, baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam.
Pia
wachimbaji hao wamesikitishwa na hatua ya watendaji kutoka Wizara ya
Nishati na Madini, kumpotosha Rais kuwa makontena yaliyozuiwa bandarini
yana mchanga wa dhahabu, badala ya mchanga wenye madini mengine, ikiwa
ni pamoja na shaba, chuma, salfa, mercury na nickel.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kiongozi wa wachimbaji wa
madini ya nickel kutoka Dodoma, Thobias Rweyemamu, alisema tangu Machi
2, mwaka huu walizuiwa kusafirisha mchanga na mawe jambo ambalo
limewasababishia hasara kubwa.
Alisema hata shughuli za uzalishaji katika maeneo ya machimbo zimesimama na kusababisha hasara ya Sh milioni 4 kila siku.
“Tunapata
hasara kubwa tangu Machi 2, tunapoteza Sh milioni 4 kila siku,
wachimbaji waliokuwa wanaendelea na shughuli zao wamesimama, hali
imekuwa ngumu, tutashindwa kuendesha maisha, familia zetu zinatutegemea
na kundi kubwa la vijana migodini… hali hii ikiendelea tutawafanyaje?” alihoji Rweyemamu.
Alisema
hadi sasa wachimbaji wadogo zaidi ya 110 wamezuiliwa, huku mchanga
wenye nickel zaidi ya makontena 60 na copper makontena saba yakiwa na
mchanganyiko wa madini yamezuiliwa.
Rweyemamu
alisema kutokana na hali hiyo, bado wanaingia hasara ya kulipia ushuru
wa Dola za Marekani 20 kila siku ambazo ni sawa na Dola 12,000 kwa
mwezi jambo linalowatia gharama kubwa.
Alisema
wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa miaka mingi, baada ya kupata
vibali halali kutoka Wizara ya Nishati na Madini na wapo kihalali si
kama ilivyoelezwa.
Mchimbaji
mwingine, Paul Kaliyemba, alisema Rais Magufuli alipotoa agizo hilo,
hawakupaswa kuchanganywa na maelezo ya wataalamu wa wizara.
Kaliyemba
alisema wanafanya biashara hiyo kihalali, hata wizara inatambua kwa
sababu leseni zilitolewa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
na walifanya ukaguzi na kujiridhisha.
Alisema
kutokana na hali hiyo, wamemwandikia barua Rais Magufuli kupitia Wizara
ya Nishati na Waziri Mkuu kupitia upya uamuzi wao na wachimbaji wadogo
waruhusiwe kuendelea na biashara yao.
Kuibuka
kwa wachimbaji hao, kumetokana na Rais Magufuli kupiga marufuku
usafirishaji wa mchanga wenye madini ya dhahabu kwenda nje ya nchi.
Kutokana
na agizo hilo, Rais Magufuli aliagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
kuzuia makontena 262 yenye mchanga unaodaiwa kuwa na madini
usisafirishwe kwenda nje ya nchi.
Mkurugenzi
wa Bandari ya Dar es Salaam, Deusdedit Kakoko, alisema baada ya Rais
kushuhudia makontena hayo, Alhamisi iliyopita walianzisha operesheni
maalumu na kubaini makontena 262 yaliyokuwa na mchanga wa dhahabu tayari
kwa kusafirishwa nje.
Alisema
makontena hayo ni mali ya mgodi wa Buzwagi, unaomilikiwa na Kampuni ya
Acacia yaliyokuwa yamehifadhiwa bandari kavu ya Mofed iliyopo Kurasini,
Temeke.
Hata
hivyo, Meneja Uhusiano wa Acacia, Asa Mwaipopo, alisema makontena hayo
ni ya mchanga wa madini ya shaba na yalifikishwa bandarini kabla ya zuio
la Rais Magufuli.