KIONGOZI
wa Kundi la Kigaidi la Waasi la ADF nchini Uganda, Jamil Mukulu
amedai hataki kurudishwa kwao kwa sababu hana imani na mahakama yoyote
nchini Uganda.
Anadai
anaamini kesi yake ikisikilizwa nchini humo hawezi kutendewa haki ni
bora ikasikilizwa katika mahakama yoyote lakini si huko.
Mukulu
alidai hayo kwa kupitia Wakili wake Martin Rwehumbiza ambaye
aliwasilisha hoja hizo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele
ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.
“Mheshimiwa
hakimu naomba mteja wangu asirudishwe Uganda, kesi yake isikilizwe
mahali popote lakini siyo nchini Uganda, nina kila sababu ya kuamini
kwamba hatatendewa haki,”alidai Rwehumbiza.
Alidai
mteja wake kwa takribani miaka 20 amekuwa akikimbia kimbia nchini humo
kutokana na utofauti aliokuwa nao na serikali ya nchi hiyo kutokana na
itikadi za kisiasa hivyo ana kila sababu ya kuamini hakuna mahakama ya
Uganda itakayosikiliza kesi yake na kumtendea haki.
Akijibu
hoja hizo Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki alidai upande wa
Jamhuri ulidhani mshtakiwa angekana kuhusika katika mauaji kuliko kuanza
kueleza kwamba anatofautiana na Serikali ya Uganda.
Alidai
kuhusu suala la mshtakiwa kutotendewa haki kuna barua kutoka Uganda
inayomuhakikishia kuwa anakabiliwa na makosa ya mauaji na yapo kwa
mujibu wa sheria na si siasa.
“Upande
wa mashtaka hatuwezi kufanya kazi kwa dhana, hiyo barua imeihakikishia
mahakama Uganda mshtakiwa atatendewa haki, mauaji hayana mahusiano na
masuala ya kisiasa, naomba mahakama itilie maanani maombi yetu,”alidai.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili iliahidi kutoa uamuzi wa mshtakiwa kurudishwa Uganda ama la Juni 12.
Awali
inadaiwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na kesi namba AA16/2015 ya mauaji
ambapo anashtakiwa pamoja na wenzake kuwa kati ya Mei, 2014 na Februari
2015 katika Wilaya ya Mayuge, Namanyingo na Bugiri washtakiwa waliwaua
baadhi ya watu maarufu wa Uganda.
Aliwataja
watu hao kuwa ni Sheikh Ductoor Abduladir Mwaya, Tito Okware, Askari
Polisi mwenye namba 54812 Babale Muzamir, Polisi mwenye namba 1404 SPC
Kemywa Karim, Polisi namba 44957 Koplo Owol Julius, Macho Stevena na
Owol John Steven.
Alidai
watu hao waliuwawa kwa kupigwa risasi na baada ya tukio hilo Polisi wa
Uganda waliwakamata washtakiwa Salim Alli Yahya, Sharif Abdallah, Mussa
Mukudanchu Nabangi, Adam Amisi, Abdulmalik Kabaale na Kabalribwe Ally.
Waliokamatwa
walikiri kuhusika na mauaji, pia walikiri kuwa ni waasi wa ADF ambalo
Uganda lilihalalishwa kuwa ni kundi la kigaidi, walikubali kuua kwa
maelekezo ya Mukulu ambaye ni kiongozi wa kundi hilo la waasi.
0 comments:
Chapisha Maoni