MOTO
mkubwa umezuka na kuteketeza nyumba zaidi ya 50 katika kisiwa cha
Kasalazi kilichopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani
Mwanza.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku, linadaiwa kuwa ni la nne kutokea kisiwani humo katika miaka ya karibuni.
Imeelezwa kuwa moto huo ulizuka na kuteketeza nyumba hizo huku wamiliki wake wakiwa kwenye shamra shamra za Krismasi.
Nyumba
zilizoteketea kwa moto ni zile zilizojengwa kwa kutumia mabanzi ya
miti, mbao na kuezekwa kwa maturubai, nyasi na baadhi kwa bati.Chanzo
cha moto huo bado hakijafahamika.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasalazi, Andrew Mkama, amesema
kuwa wakati tukio hilo linatokea, wakazi wengi wa kisiwa hicho walikuwa
kwenye kumbi mbalimbali za starehe kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu
Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.
Mkama
alisema alilazimika kupuliza filimbi kuashiria hatari na wananchi
walijitokeza na kuanza jitihada za kuuzima moto huo licha ya kwamba
tayari ulikuwa umeshasababisha madhara makubwa kwa kuunguza mali zote
zilizokuwa ndani yake.
Hata hivyo alisema hakuna mtu aliyekufa wala kujeruhiwa kutokana na janga hilo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema moto huo umesababisha hasara kubwa kwao.
Mmoja
wa mashuhuda hao, Raphael Bituro, anayemiliki duka la vinywaji, alisema
baada ya kupulizwa filimbi kuashiria hali ya hatari, baadhi ya wateja
wake walikurupuka bila kulipia vinywaji vyao na hivyo kusababisha apate
hasara.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alithibitisha kisiwa hicho kuungua kwa moto.
Kipole
alisema ameagiza kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini ukubwa wa madhara
hayo na kuahidi kutoa taarifa zaidi atakapopewa ripoti hiyo.
Kisiwa
hicho kinakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 2,400 ambao hujihusisha na
shughuli za uvuvi na ni miongoni mwa visiwa vinane vilivyopo kwenye Kata
ya Bulyaheke wilayani Sengerema.