Baada
ya kuripotiwa taarifa kwamba kuna uhaba wa kinga za ugonjwa wa
Pepopunda kwenye Hospitali za Dar es salaam, Leo January 2, 2017 Wizara
ya Afya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wazee na watoto imetoa ufafanuzi
kuhusu chanjo hiyo na kueleza kuwa ipo akiba ya kutosha tofauti na
ilivyoandikwa na gazeti la Tanzania Daima leo Jumatatu ya tarehe
02/01/2017.
Wizara
ya Afya imesema kuwa habari iliyotolewa na gazeti hili sio sahihi, na
hata majina ya watu waliohojiwa kuhusu kuadimika kwa chanjo hiyo hawapo
wizarani, na wengine wapo masomoni, hii ni taarifa yazamani sana
kimsingi imepitwa na wakati ambayo haikupaswa kutolewa kama wahariri wa
habari wangekuwa makini katika kufanyia kazi taarifa hii.
Kwenye
taarifa hiyo ametajwa Daktari kiongozi wa hospitali ya Amana, Stanley
Dinagi, ambaye sasa hivi hayupo nchini, yupo masomoni. Pia katajwa
Mganga mkuu wa serikali Donald Mmbando ambaye hayupo katika wadhifa huo
sasa imepita takribani miaka mitatu iliyopita.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano
Serikalini-Afya, Nsachris B. Mwamaja imefafanua uwepo wa kinga hiyo
katika wilaya kuu tatu za Dar es salaam.
Mkoa wa Dar Es Salaam una chanjo za Pepopunda zakutosha katika manispaa zake zote na umesambaza mgao wake kama ifuatavyo,
- ILALA – Dozi 35,300 zilisambazwa Tarehe 06/12/2016 na mahitaji yao kwa mwezi Dozi 7,110.
- TEMEKE – Dozi 33,000 zilisambazwa Tarehe 06/12/2016, mahitaji yao kwa mwezi ni Dozi 7,620.
- KINONDONI – Dozi 11,000 zilisambazwa Tarehe 07/12/2016, mahitaji yao kwa mwezi ni dozi 9,210.
“Kwa
hivi sasa hakuna upungufu wowote wa chanjo ya pepopunda nchini, Tuna
jumla ya dozi 599,000 katika bohari ya taifa, na tunatarajia kupokea
shehena nyingine ya dozi 1,200,000 wakati wowote ili kuhakikisha kwamba
hatuna uhaba wa chanjo hii.” – Mwamaja