WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaonya wakazi wa Ruangwa wanaokata miti kwenye
misitu waache kufanya hivyo mara moja ili kuokoa ardhi chepechepe
waliyokuwa nayo.
Amesema
ukataji miti huo unafanywa zaidi na watu wanaoanzisha mashamba ya ufuta
na wapo walioamua kulima karibu na vyanzo vya maji hali iliyosababisha
maji yakauke kwenye maeneo mengi.
“Zamani
kuna maeneo ulikuwa haupiti hadi ukunje suruali, na kama una gari napo
pia ilikuwa ni taabu kupita kwenye maeneo hayo. Lakini sasa hivi, hakuna
tena maeneo hayo ndiyo maana kila unakopita unakuta akinamama
wanatembea mwendo mrefu na ndoo huku vijana wakibeba madumu kwenye
baiskeli nao wakitafuta maji,” alisema Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa
jimbo la Ruangwa.
Ametoa
onyo hilo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa vijiji
mbalimbali vya wilaya hiyo ambao walifika Ruangwa mjini kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM kusikiliza taarifa ya
mambo aliyoyafanya jimboni humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
“Kilimo
cha ufuta kimekuwa balaa, sasa hivi hakuna maji sababu ya ukataji miti
ovyo. Mfano mzuri ni mto Mbwemkuru ambao ulikuwa ukitiririsha maji mwaka
mzima, angalia sasa hivi, umegeuka kuwa mto wa msimu na chanzo ni
ukataji wa miti,” alisisitiza.
“Tusipobadilika
na kuacha hiyo tabia tutamlaumu mbunge na Serikali kuwa hawaleti maji
wakati sisi wenyewe tumechangia hali hiyo kwa kuharibu vyanzo vya maji,”
alionya na kuongeza kuwa amelazimika kutafuta mashine ya kuchimba maji
ili kupunguza tatizo la maji.
Alisema
mapema mwaka huu, wataalamu wataanza kufanya utafiti ili kubaini maji
yako umbali gani kwenda ardhini kabla ya kuanza kuchimba visima hivyo.
“Ikibidi tutaaza na visima vifupi na vya kati ili maji yapatikane
haraka,” alisema.
Akielezea
mipango ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, Waziri Mkuu aliwaeleza
wakazi wa jimbo hilo kwamba anatamani kuona kila kijiji kinakuwa na
zahanati ili kupunguza umbali wa upatikanaji wa huduma za afya kwa
wakazi wa vijijini.
“Kila
nilikopita vijijini nimewahamasisha wananchi waanze kufyatua mafotali
ili ujenzi wa boma ya zahanati uanze. Na mimi nimeahidi kuchangia mabati
kwa kila zahanati, na kuna baadhi ya maeneo nimechangia hata mabati ya
nyumba ya mganga na muuguzi,” alisema.
Alisema
mwaka uliopita, alifanikiwa kukamilisha ujenzi wa wodi ya akinababa, ya
akinamama na kukarabati wodi ya magonjwa mchanganyiko katika hospitali
ya wilaya ambapo fedha taslimu milioni 100 zilitumika. Pia aliwezesha
kufunga umeme wa jua kwenye zahanati zote zinazotoa huduma za afya ndani
ya jimbo na kazi hiyo itaendelea kwa awamu ya pili.
“Pia
niliweza kulipia kaya 10 zisizokuwa na uwezo kwa kila kijiji ili
zijiunge na mfuko wa afya ya Jamii (CHF) kwa gharama za shilingi milioni
9. Jumla ya vijiji 92 vimefikiwa. Ninawasihi wana-Ruangwa kila mmoja
ajiunge na mfuko huu ili muweze kupatiwa huduma za afya bila matatizo,”
aliongeza.
Akielezea
kuhusu sekta ya elimu, Waziri Mkuu alisema ameweza kufadhili ujenzi wa
matundu ya vyoo 70 Katika shule za msingi saba ambapo kila shule
imejengewa matundu 10 (manne wavulana, manne wasichana na mawili kwa
walimu) ambapo jumla ya sh. milioni 63 zimetumika. Alisema kazi hiyo
itaendelea awamu ya pili.
“Zaidi
ya hayo, nimefanikisha ufungaji wa umeme jua kwenye shule za sekondari
nne za Chunyu, Makanjiro, Narungombe na Nambilanje. Katika awamu ya
kwanza tumekamilisha kuweka umemejua kwenye sekondari za tarafa ya
Mandawa, na tarafa ya Ruangwa imefikiwa nusu tu. Katika awamu ya pili,
tutamalizia tarafa ya Ruangwa na kukamilisha tarafa nzima ya Mnacho,”
alisema.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, JANUARI 2, 2017.