test

Jumatano, 18 Januari 2017

CCM Yamvaa LOWASSA Sakata la Uhaba wa Chakula Nchini


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuna mwanasiasa mmoja ambaye hana nyenzo yoyote za kupata taarifa za uhakika ambaye amekuwa akiwaeleza na kuwaaminisha wananchi kuwa kuna tatizo la njaa ili kuzua taharuki. 
Polepole alisema baadhi ya wanasiasa wanaotangaza baa la njaa wana lengo la kuichonganisha Serikali na wananchi. 
Pamoja na kutomtaja jina, hivi karibuni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiwa katika kampeni za udiwani mjini Bukoba alikaririwa akisema, “Serikali imesema haitoi chakula, mimi nimejadiliana na chama changu tumeona tufanye mpango wa kuwatafutia chakula Watanzania. Hata kama ni kutoka nje ya nchi ninaamini dunia itatusikia.” 
Jana, akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa Serikali ya CCM katika kipindi cha mwaka mmoja, Polepole aliwataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wanaoleta maneno yasiyo sahihi na yaliyojaa upotoshaji kwa Serikali. 
“Sipendi kujadili watu hapa, lakini sielewi huyu malengo yake ni nini? Tunacho chakula na imani ya CCM ni kujitegemea, ndiyo mwelekeo wa chama hiki,” alisema.
 Alieleza kuwa duniani kote kuna utaratibu unaofahamika bayana na kuwa baa la njaa siyo kitu kidogo, ni jambo kubwa na nchi inapokumbwa, mkuu wa nchi ndiye mwenye dhamana ya mwisho kutangaza. 
Polepole alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanajitegemea na siyo kuwa ombaomba..., “Lakini anatokea kiongozi mmoja anawaahidi kuwa ataenda kuwaombea chakula cha bure. 
"Imeandikwa asiyefanya kazi na asile. Watanzania hawa wametutuma tuwawekee mazingira mazuri ili wafanye kilimo na biashara.
“Kiongozi anayesema nitaleta chakula cha bure na watu wasifanye kazi ni bahati mbaya sana. Imani yetu ni kubwa, Watanzania hawa wanaona mambo haya.” 
Aliwataka Watanzania kuwapuuza viongozi wa aina hiyo aliosema wanafahamu utaratibu lakini wameamua kuleta upotoshaji wa kutoa taarifa zisizo sahihi. 
Polepole aliishukuru Serikali kwa kufafanua vyema sakata hilo akisema kuna tani milioni 1.5 za chakula zitakazosambazwa sehemu mbalimbali zilizokumbukwa na ukame. 
 Alisema Awamu ya Tano, itaendelea kuishi katika misingi yake kwa kusema ukweli daima na fitina kwake mwiko. 
“Nilitarajia viongozi wote bila kujali itikadi, tungeendelea kuhamasisha wananchi kutunza nafaka na kufanya kazi kwa bidii. Hili siyo jukumu la Serikali,” alisema. 
Pia aliwataka wanasiasa wa upinzani kuacha kutumia matatizo yanayowapata wananchi kama mtaji wa kisiasa ikiwamo tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Mbali na hilo la njaa, Polepole alizungumzia mwaka mmoja wa Rais John Magufuli na kusema amefanikiwa kutatua kero mbalimbali zilizokuwa zikilalamikiwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015. 
Alisema miongoni mwa kero hizo ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kutimiza imani ya CCM inayosema binadamu wote ni sawa hasa katika huduma za kijamii kwenye elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. 
Alisema katika mwaka wa masomo unaoendelea sasa, vijana na watoto 20,000 wanakwenda kusoma elimu ya juu na watapata uwezeshaji wa Serikali wa kuendelea na masomo yao. 
“Huu ni mwaka wa kwanza, ambao kidesturi ni wa kujipanga lakini Serikali ya Rais Magufuli imeamua kutekeleza maendeleo kwa Watanzania huku ikiendelea kujipanga na kunyoosha nchi,” alisema Polepole.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx