Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekabidhi vitu vyenye thamani
ya zaidi ya Sh milioni 164 alivyoahidi kwenye ziara zake na pikipiki
tano kwa Saidi Mrisho aliyetobolewa macho na ‘Scorpion’.
Kuanzia Novemba 19 hadi 28, Makonda alifanya ziara katika wilaya za Dar es Salaam kujua matatizo ya wananchi na kuahidi kutekeleza baadhi ya mambo.
Akizungumza
jana, Makonda alisema ameona ni vema akaanza kutekeleza baadhi ya ahadi
zake kabla mwaka kumalizika, huku mambo mengine yakisubiri utekelezaji
kutoka ngazi za juu za uongozi.
Makonda alikikabidhi kituo cha kurekebisha tabia cha Kigamboni magodoro 50, runinga, king’amuzi, mitungi miwili ya gesi na jiko.
Pia
alikabidhi gari la kubeba wagonjwa kwa Jeshi la Polisi Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU) Ukonga, na tumba za kwaya ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ).
Sekondari
ya Jitegemee ilipewa mabati 2,000, shule ya msingi Mbagala Annex mabati
1,000, shule ya Katoliki mifuko 10,000 ya saruji, soko la samaki
Msasani mabati 300, kanisa la AIC matofali 10,000 na mabati 200 kwa
ajili ya Uwanja wa Taifa.
Katika
kuthamini viongozi wanaojituma, alitoa pikipiki kwa mtendaji wa kata ya
Mbuyuni na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buguruni.
Pia
hakuwaacha nyuma wajasiriamali kwani alimkadidhi Lumino Evance mtaji wa
Sh milioni moja na mama muuza machungwa Zuhura Waziri mtaji wa Sh
200,000.
Kutokana
na changamoto ya maji Ukonga, Makonda alikabidhi Sh milioni 13 ili
wananchi wa Gongo la Mboto na Pugu wapate maji. Pia alitoa Sh 500,000
kwa ajili ya kukamilisha tangi la maji kwa wananchi wa Buyuni, kata ya
Pemba Mnazi.
Aidha,
Makonda alitoa zawadi kwa watumishi wanne waliokuwa tayari kujitolea
na kufanya kazi kwa ufanisi, ambao walizadiwa kulala siku moja kwenye
hoteli ya kifahari kwa gharama ya zaidi ya Sh milioni tano.
Kuhusu
Mrisho ambaye alishindwa kuhudhuria hafla hiyo na kuwakilishwa, Makonda
alisema utaratibu wa kumtafutia nyumba kama alivyoomba unaendelea.
Aliongeza
kuwa kilichokwamisha ni eneo alilochagua ambalo walikuta lina mgogoro,
hivyo alisema wanamtafutia sehemu nyingine kwa sasa.
Baada ya makabidhiano hayo baadhi ya wanufaika walimshukuru Makonda kuwa mwenye moyo wa uthubutu.
Kamanada
wa FFU Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Stanley Kukaganeo alisema gari
walilokabidhiwa litasaidia kuokoa maisha ya wananchi wengi wanaohitaji
msaada wa dharura.
“Tumekuwa
tukiumia sana mgonjwa kufia mikononi mwetu kwa sababu ya kukosa gari la
kumwahisha hospitali ila Mkuu wa Mkoa tulikueleza hilo na sasa
umetekeleza, ahsante sana,” alisema.
Zuhura alisema hakuwahi kufikiria kitu kama hicho katika maisha yake na anaona ni bahati kupata msaada huo.
“Niliomba Sh 20,000 ila wewe (Makonda) umenipa Sh 200,000, Mungu akubariki na uendelee na moyo huo huo wa kutusaidia,” alisema.
Kamanda
wa kikosi cha kutuliza ghasia kanda maalum ya Dar es Salaam,
Acp.Stanley Kulyamo akipokea gari la wagonjwa kutoka kwa mkuu wa mkoa wa
Dar es Salaam ,Paul Makonda jana Jijini Dar es Salaam.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam , Paul Makonda akikabidhi zawadi tumba kwa
ajili ya bendi ya jeshi la Wananchi mara baada ya kufanya vizuri katika
mahadhimisho ya miaka 55 ya uhuru.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda , akikabidhi shilingi laki
mbili kwa mjasiliamali ,Zuhura Waziri mkazi wa Mwembe Yanga kwa ajili ya
kuongeza mtaji wake wa Supu.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda akikabidhi mifuko ya Saruji kwa
Mkuu wa shule ya St Joseph Goba , Sister Caroline Kokutekana, kama
sehemu ya kutimiza ahadi yake wakati wa mahafali ya shule hiyo.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam ,Paul Makonda akikabidhi mabati kwa mkuu wa
shule ya sekondari Jitegemee kama sehemu ya ahadi yake katika kampeni
ya Dar es Salaam mpya.