Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, ametaka vijana wa chama hicho
kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia aliodai unafanywa na
watawala.
Alisema hayo juzi alipokutana na vijana wa chama hicho ambao ni wanavyuo (CHASO) wa vyuo vikuu mkoani hapa.
Lowassa
ambaye yuko Tabora kwa ziara ya kuimarisha chama, aliwataka vijana hao
kuwa na ujasiri wa kukabiliana na ukandamizaji wa demokrasia kwani
vijana duniani ndio chachu ya mabadiliko.
“Nimekuja
Tabora kuwashukuru kwa kura nyingi mlizonipigia na hamasa kubwa
mliyoionesha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Katika uchaguzi ule
tulishinda, lakini ushindi mkubwa zaidi ni tulipofanikiwa kuvumilia na
kuweka maslahi ya watoto, wazee na mama zetu mbele," alisema na kuongeza:
"Amani
ni tunu muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa kuliko kitu kingine
chochote. Msikate tamaa, tumejipanga vema kwa uchaguzi ujao wa mwaka
2020 na hatutadhulumiwa tena haki yetu, kama ilivyokuwa mwaka jana,” alisema Lowassa.
Lowassa
ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani, alisema Jambo Kuu na la msingi ambalo
wana Chadema wanatakiwa kuwa nalo sasa katika chama ni umoja na
mshikamano kati yao.
"Umuhimu
wa umoja na mshikamano ndani ya chama chetu ni mkubwa sana, hasa katika
kipindi hiki ambacho Serikali inajaribu kwa kila namna kukandamiza
Upinzani na demokrasia na jambo hili si geni, ukirudi nyuma katika
historia ya vyama vya siasa nchini, hata kabla ya Uhuru, unaweza kuona
umoja ulivyoisadia TANU dhidi ya chokochoko za chama alichoanzisha
mkoloni wakati ule - United Tanganyika Party (UTP) kukabiliana na
kuidhoofisha TANU na kumzuia Mwafrika kupata Uhuru na kujitawala," alisema.
Aliwaambia
vijana kwamba changamoto kama hizo ni za kawaida kwa vyama vingi vya
upinzani hasa Afrika, ambavyo vinaungwa mkono na wananchi wengi
wakiamini ni vya ukombozi.
Lakini
pia alisema katika kujenga umoja na mshikamano huo ndani ya chama, ni
lazima nguvu kubwa ipelekwe kwenye matawi waliko wananchi.
"Katika
chama chochote cha siasa watu wengi hawako ngazi za juu, bali
mashinani. Ni lazima nguvu yetu kubwa ielekezwe huko kwa sasa, ili
kuhakikisha chama kinakuwa na misingi madhubuti ambayo inaweza kutumika
kukisaidia nyakati za uchaguzi," alisema.
Aidha,
Lowassa ambaye katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana alipata asilimia 38
ya kura, alihoji umuhimu wa Serikali kununua ndege zaidi, kuliko
kupeleka huduma muhimu vijijini.
"Tumesikia
nia njema yao ya kuagiza ndege nyingine zaidi miaka miwili ijayo,
lakini tunajiuliza, je isingekuwa busara kutumia fedha hizo kupeleka
maji safi na salama mijini na vijijini?" Alihoji.