Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana iligeuka kuwa uwanja wa masumbwi,
baada ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) kupigana na kusababisha
watu watatu kujeruhiwa.
Wafuasi
hao ni wa Bodi ya Wadhamini ya Chama walio upande wa Katibu Mkuu,
Maalim Seif Sharif Hamad na wanaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho,
Profesa Ibrahim Lipumba.
Tukio
hilo la aina yake, lilitokea kabla ya kuingia kwenye chumba cha
mahakama, tayari kwa kusikiliza uamuzi wa kujitoa au kuendelea kwa Jaji
Sekiet Kihiyo kusikiliza kesi hiyo na baada ya kutoka mahakamani.
Hata
hivyo, Jaji Kihiyo alitupilia mbali maombi ya bodi ya wadhamini kwamba
asiendelee na kesi hiyo, kwa madai kwamba hawana imani naye, kwa kusema
kuwa maombi hayo, hayana msingi kwa kuwa sheria inamruhusu kutojitoa
kirahisi kwenye kesi.
Alieleza
kuwa wadau hawana nafasi kujichagulia jaji wanayemtaka. Kabla ya
kuingia kwenye chumba cha mahakama, mfuasi mmoja wa Profesa Lipumba na
wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Maalim Seif, walianza kurushiana ngumi na
kuleta mtafaruku katika eneo la watu wanaosubiria kesi zao kuitwa huku
Lipumba akionekana kulindwa na walinzi mbalimbali.
Aidha,
baada ya jaji kutoa uamuzi huo, wafuasi wote walitoka nje, ambapo
wakati Profesa Lipumba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi
hiyo, wafuasi hao walianza kupigana na kujeruhi watu watatu, ambapo
mmoja wao, aliyejulikana kwa jina la Robert Samson, alijeruhiwa kwa
kutumia kitu chenye ncha kali shingoni na kusababisha kuvuja damu
nyingi.
Hali
hiyo iliendelea kwa wafuasi wa bodi ya udhamini, kulalamikia walinzi wa
mahakama, kwamba ni kwa nini wanakagua watu, lakini wameshindwa kuwaona
wenye silaha, ikiwemo visu na kusababisha watu wao kujeruhiwa.
Pia
walidai kuwa licha ya kuwepo kwa askari wengi mahakamani hapo wakiwa na
silaha, walishindwa kutuliza ghasia hiyo, ambayo imeleta madhara, kwa
kuwa kila mfuasi aliyemuona adui yake alishikana naye shati na kupigana.
Kabla
ya vurugu hizo kuisha, Profesa Lipumba na wafuasi wake walipanda magari
yao huku wakimwimbia nyimbo za kumsifu mwenyekiti huyo na kuondoka.
Waliwaacha wafuasi wa bodi ya wadhamini, wakilalamikia kitendo cha
kupigwa.
Walijiapiza
kwamba watajipanga ili siku kesi hiyo itakapoitwa tena, watahakikisha
wanawadhibiti wapinzani wao na kwamba wataleta madhara makubwa
mahakamani hapo.
Awali,
akitoa uamuzi huo, Jaji Kihiyo alisema kuwa Novemba 10 mwaka huu,
mawakili wa bodi ya wadhamini ya CUF, wakiwakilishwa na Rahim Khalfan,
waliandika barua kwa Msajili wa mahakama hiyo, kuomba jaji huyo ajitoe,
kwa kuwa wateja wao hawana imani naye.
Alisema
kuwa hawezi kujitoa, kwa sababu zisizo za msingi, kwamba anaupa
upendeleo upande wa washitakiwa na kuwaacha waombaji wakati hakukuwa na
mazingira ya kuruhusu kutolewa hoja kwa pande zote.
“Mahakama
ya Rufaa inasema majaji au mahakimu hawatakiwi kujitoa kwa urahisi
kwenye kesi. Pia sheria hairuhusu wadau ambao wanakuja kwa mara ya
kwanza mahakamani na hawajui taratibu za mahakama watake kujichagulia
jaji,” alisema Jaji Kihiyo.
Alisisitiza
kuwa jaji au hakimu ana mamlaka chini ya sheria, kujitoa au kuendelea
kusikiliza shauri, kama ataridhika kwamba sababu zilizotolewa, zina
nguvu ya kushawishi afanye hivyo.