Bodi
ya Wakurugenzi ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) imewaondoa katika
nyadhifa zao wakurugenzi wote waliopo katika menejimenti na baadhi ya
mameneja, baada ya kubainika kuwa na kasoro za kiutendaji na kielimu.
Uamuzi
huo, ambao hautamhusisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Ladislaus
Matindi, ulitolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 18, lengo likiwa
ni kuboresha muundo wa ATCL, ili kukidhi matakwa ya muda mfupi wakati
muundo wa kudumu ukiandaliwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya shirika hilo,
Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi Emmanuel Korosso, alisema katika
kikao hicho bodi iliamua kuwaengua wakurugenzi watano waliokuwa katika
idara mbalimbali, ikiwamo ya biashara, ambayo ilikuwa na kaimu.
Mhandisi
Korroso alitaja idara nyingine ambazo wakurugenzi wameondolewa kuwa ni
fedha, usalama, ufundi na uendeshaji, ambayo mkurugenzi wake alikuwa
anaelekea kustaafu.
“Kwakuwa
wakurugenzi wengi walikuwa wanakaimu nafasi hizo, tumeamua wakurugenzi
wanaokaimu warudishwe katika nafasi zao za chini, ambazo si
menejimenti au wahamishiwe katika vituo vya mikoani,” alisema Mhadishi
Korosso.
Alisema
bodi pia imeagiza kuondolewa kabisa katika shirika hilo wakurugenzi na
mameneja waliothibitishwa ili waweze kupangiwa majukumu mengine
yatakayoendana na sifa walizonazo.
Alisema
kikao hicho pia kimemuagiza Mtendaji Mkuu kutangaza mara moja nafasi za
wakurugenzi na mameneja zilizo wazi kwa kufuata muundo uliopitishwa.
Mbali
na hilo, Mhandisi Korosso alisema kwa sasa shirika hilo limeweza
kuongeza nidhamu katika mapato na matumizi, jambo ambalo limechangia
kuanza kulipa baadhi ya madeni wakati Serikali ikisubiri uhakiki
umalizike ili iweze kuyachukua.
“Tumeweza
kudhibiti mapato na matumizi vizuri, kumekuwa na ongezeko la mapato ya
uzito wa ziada wa mizigo kutokana na usimamizi mzuri, ukusanyaji wa
mapato kutoka vituoni na mawakala umeboreshwa sana kutokana na
ufuatiliaji wa karibu wa mauzo,” alisema Mhandisi Korosso.
Aliongeza
kuwa, bodi pia imetoa ruhusa kwa wafanyakazi na familia zao kupewa
tiketi bure mara moja kwa mwaka kama stahiki ya likizo na tiketi yenye
punguzo mara moja kwa mwaka.
Kampuni
ya ATCL, ambayo awali ilikuwa haina ndege hata moja, ilianza kufanya
kazi za safari za ndege Oktoba 14, mwaka huu, baada ya Serikali kununua
ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q400.