test

Jumatatu, 19 Desemba 2016

Rais Magufuli Afanya Uteuzi Wa Wakuu Wa Wilaya Wawili Na Wakurugenzi Watatu .........Nafasi ya Humphrey Polepole yachukuliwa na Kisare Makori


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 19 Desemba, 2016 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 2 na Wakurugenzi 3 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Kisare M. Makori kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Bw. Kisare M. Makori anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Humphrey Polepole ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Avod Mmanda Herman kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara iliyopo katika Mkoa wa Mtwara.

Bw. Avod Mmanda Herman anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Khatib M. Kazungu ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Ramadhan Geodrey Mwangulumbi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga iliyopo Mkoani Shinyanga.

Bw. Ramadhan Geodrey Mwangulumbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Lewis Kalinjuna ambaye anastaafu kwa mujibu wa Sheria.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw Rojas John Romuli kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda iliyopo katika Mkoa wa Katavi.

Bw. Rojas John Romuli anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ngalinda Hawamu Ahmada aliyefariki dunia hivi karibuni.

Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Rashid K. Gembe kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga iliyopo katika Mkoa wa Tanga.

Bw. Rashid K. Gembe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Mkumbo Emmanuel Barnabas ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi karibuni.

Uteuzi wa huu unaanza mara moja na wateule wote wanatakiwa kuripoti Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mara wapatapo taarifa hii.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

19 Desemba, 2016

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx