Zaidi
ya mabasi 70 ya daladala yanayosafirisha abiria katika baadhi ya njia
za manispaa ya Dodoma, yamegoma kutoa huduma kwa siku nzima ya leo
kutokana na madai ya kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani.
Daladala
hizo zinazotoa huduma kati ya Jamatini na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)
pamoja na Jamatini na Veyula, zilisimamisha huduma zake kwa siku nzima
ya leo zikipinga manyanyaso ya askari hao.
Baadhi
ya madereva wa mabasi hayo, wamesema wamechoshwa na manyanyaso kutoka
kwa askari hao kwa vitendo vyao vya kuwakamata kiuonevu.
Wamesema sababu kubwa ya mgomo wao ni rushwa na manyanyaso wanayofanyiwa na baadhi ya askari hao wa usalama barabarani.
Hata
hivyo, akijibu malalamiko ya madereva hao, Kamanda wa Kikosi cha
Usalama Barabarani mkoa wa Dodoma, Marisone Mwakyoma, amesema sheria
zipo wazi kama kuna mtu anaombwa rushwa na kutoa, wote wana makosa kwa
sababu zipo ngazi za kuripoti matukio hayo.
Afisa
Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra) mkoa wa Dodoma, Conrad Shio, amesema baada ya kutokea kwa
mgomo huo waliweza kutoa kibali kwa magari mengine kuweza kubeba abiria
wasipate shida ya usafiri.