WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za serikali zinazotumia kuni na
mkaa kwa wingi kama vile shule na majeshi kuanza mikakati madhubuti ya
kubadili mfumo wa kupikia na kuweka majiko ya gesi ili kupunguza
matumizi ya mkaa ambayo yamekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Alisema
hayo jana Dar es Salaam katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe wakati wa
ufunguzi wa warsha ya wadau kujadili namna na njia bora ya kupunguza
matumizi ya mkaa kwa usimamizi endelevu wa mazingira nchini.
“Nimeelezwa
kuwa makampuni yanayouza majiko na gesi ya kupikia aina ya LPG
yameonesha nia ya kuweka majiko haya bila gharama yoyote. Tutumie vyombo
vyetu vya habari na majukwaa ya mikutano kuhamasisha wananchi kutumia
fursa hii ya LPG,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha,
alisema nchi inakabiliwa na changamoto kubwa za uharibifu wa mazingira
kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ufugaji wa kuhamahama, mifugo
kuvamia misitu na kuiharibu pamoja na vyanzo vya maji na watu kukata
miti katika vyanzo hivyo.
Alisema
mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mabadiliko ya vipindi vya mvua,
mtawanyiko wa kiwango cha mvua na hivyo kutishia usalama wa chakula na
ukosefu wa malighafi kwa viwanda ambavyo ndiyo njia ya kuivusha nchi
kuingia katika uchumi wa kati.
Alisema
takwimu zinaonesha asilimia 90 ya nishati ya kupikia hasa mijini ni
mkaa na kwa vijijini asilimia kubwa na wananchi wanatumia kuni ambapo
takwimu hizo pia zinaonesha ili kuzalisha tani moja ya mkaa sawa na
magunia 30 zinahitajika tani 12 za kuni na hali hiyo imesababisha nchi
kupoteza zaidi ya hekta 370,000 kila mwaka.
Alisema
utafiti pia umebainisha kwamba matumizi ya mkaa yanaongezeka kutokana
na ongezeko la watu na kama haitaanza kutumika nishati mbadala, mahitaji
ya mkaa yatafikia takribani tani milioni tano kwa mwaka ifikapo mwaka
2030 kutoka tani milioni 2.4 zilizotumika mwaka 2015.
Hata
hivyo, Profesa Maghembe alisema wizara yake inatarajia kupandisha
ushuru na kodi ya mkaa ili uuzwe kwa bei ya juu lengo likiwa ni
kuwafanya wasafirishaji na wanunuzi washindwe kumudu gharama na hatimaye
matumizi ya mkaa kupungua.