Watumishi
waandamizi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
waliosimamishwa kazi baada ya kusafiri nje ya nchi kinyume na agizo la
Rais John Magufuli, wamerejeshwa kazini baada ya takriban mwaka mmoja
kupita.
Msemaji
wa Takukuru, Mussa Misalaba aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkurugenzi
wa Elimu kwa Umma, Mary Mosha na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu ambao wamerejeshwa baada ya shauri lao
kusikilizwa na ofisi husika.
“Shauri lao lilishughulikiwa na Ofisi ya Rais kutokana na vyeo vyao, wamerejeshwa ofisini na kuanza kazi Novemba 14,” alisema.
Misalaba
alisema watumishi wengine waliorejeshwa kazini ni aliyekuwa Msemaji wa
Takukuru, Doreen Kapwani na Katibu Muhtasi wa mkurugenzi mkuu, Rukia
Nikitas shauri lao lilisikilizwa na mamlaka ya taasisi hiyo na hatua za
kinidhamu zilichukuliwa ikiwamo kuhamishwa vitengo.
Watumishi
hao walidaiwa kuondoka nchini Novemba 23 mwaka jana, kabla ya kupewa
majibu ya vibali walivyoomba baada ya kuandika barua Ikulu kuhusu safari
hiyo.
Rais
Magufuli alitangaza kufuta safari za nje ya nchi kwa maofisa wa
Serikali Novemba 7, 2015 na kutoa mwongozo kwamba safari
zitakazoruhusiwa ni zile zenye ruhusa ya Ikulu.
Kusimamishwa
kwao kazi kulitangazwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue alipozungumza na waandishi wa habari Desemba 16 mwaka jana.
Takukuru
iliiandikia Ikulu barua ya kuomba kibali kwa ajili ya safari hiyo,
lakini kabla ya kujibiwa, wafanyakazi hao waliamua kusafiri.