RAIS
mteule Donald Trump wa Marekani, ametishia kufikiria upya ahadi
aliyoitoa ya kutomfungulia mashtaka aliyekuwa mpinzani wake katika
kinyang’anyiro cha urais, Hillary Clinton.
Trump
ametoa tishio hilo kufuatia taarifa kuwa timu ya kampeni ya Hillary
itashiriki kuhesabu kura upya katika Jimbo la Wisconsin, ambalo bilionea
huyo alishinda.
Uamuzi
wa timu hiyo unatokana na aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha
Kijani, Dk. Jill Stein, kuwasilisha hati ya kuhesabiwa upya kura katika
jimbo hilo.
Hili
ni pamoja na kuwa tangu mwanzo timu ya Hillary ilishasema haioni ishara
zozote za kukiukwa sheria katika kinyang’anyiro hicho cha kuingia White
House.
Msaidizi
wa Trump, Kellyanne Conway, alisema iwapo timu ya Hillary itaendelea
kushinikiza azma ya kutaka kushiriki kuhesabu kura upya, Trump hatasita
kufikiria upya ahadi aliyoitoa ya kutomchukulia hatua kutokana na
kutumia barua pepe binafsi wakati alipokuwa waziri wa mambo ya nje.
Aidha Trump alimkumbusha Hillary kuwa alishakubali matokeo na kabla ya uchaguzi pia aliahidi atakubali kushindwa.
Lakini
wakili wa masuala ya uchaguzi wa Chama cha Democratic, Marc Erik,
alisema harakati zao kuwezesha kuhesabu upya kura zitaendelea kufanyika
hata katika majimbo mengine mawili ya Michigan na Pennsylvania.
Hata
hivyo, wataalamu wa masuala ya uchaguzi walisema kutokana na matokeo ya
jumla kuonyesha Hillary alikuwa nyuma ya Trump kwenye majimbo mengi,
itakuwa ngumu kubatilisha ushindi.
Tisho la kambi ya Trump limeenda sambamba na bilionea huyo kudai kwamba watu milioni mbili walipiga kura kinyume cha sheria.
Alitoa
kauli hiyo kufuatia Hillary kuongoza kwa pengo la kura za wananchi
milioni 2, lakini ni Trump ameibuka mshindi kwa kupata kura nyingi za
wajumbe kuliko mpinzani wake.
Trump
pia alidai kulitokea ulaghai mwingi katika upigaji kura majimbo ya
Virginia, New Hampshire na California ambako Hillary alishinda.
Na aliwashutumu wanahabari wa Marekani akisema wamekataa kuangazia suala hilo.