Sakata la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka fedha katika akaunti
maalumu kwenye benki za biashara limechukua sura mpya baada ya Gavana wa
Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kusema si kosa kisheria.
Profesa
Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRA iliyovunjwa na Rais
John Magufuli Jumapili iliyopita, alisema mjini Arusa jana kuwa hakuna
hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum isipokuwa hilo suala
lilikuwa na hali nyingine.
Japokuwa Profesa Ndulu hakutaka
kufafanua zaidi kwa maelezo lilichomekewa tu katika mkutano na waandishi
wa habari wa kuelezea hali ya uchumi, alisema hali hiyo ndiyo suala
lililozungumzwa na siyo kusema “fixed deposit account” ni mbaya.
“Kwani amesema fixed account zote ni mbaya, pamoja na za watu binafsi?
Ndo hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa hiyo nilikuwa tayari,”
alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa
Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari
walipotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka fedha
kwenye akaunti maalumu tena benki binafsi.
Kauli hii ya Profesa
Ndulu imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kueleza kilichochangia
kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi, Bernard
Mchomvu na pia kuivunja bodi yake iliyokuwa na wajumbe tisa. Kati ya
wajumbe hao tisa, watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na wanne ni wa
kuteuliwa.
Wajumbe wanaoingia kwenye Bodi kwa mujibu wa sheria
ni Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu; Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo
Kidata; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Doto James;
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar, Khamis Mussa Khamis; na Katibu
Mkuu Mipango. Bodi hiyo ilivunjwa Jumapili iliyopita.
Rais
Magufuli alisema juzi kuwa Bodi ya TRA iliyokuwa na watendaji hao wakuu
wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi wa
menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.
“Juzi
hapa tumekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya
matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit
account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela
nikazichukua na bodi kwaheri,” alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni
rasmi kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
yaliyofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambako jumla ya watu 4038
walihitimu shahada mbalimbali
Ukwasi wa mabenki
Katika hatua nyingine
Profesa Ndulu amesema ukwasi wa fedha katika mabenki umeshuka
ikilinganishwa na kipindi cha nyuma hatua inayotatiza utoaji wa mikopo
ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Akizungumza jana na
waandishi wa habari mara baada ya kufungwa mkutano wa 18 wa taasisi za
fedha uliofanyika kwa siku mbili jijini Arusha alisema hali hiyo
inafanyiwa kazi na wadau wa taasisi hizo ili kuja na mbinu kufanya kuwa
endelevu kwani uchumi unategemea uwekezaji unaotegemea mikopo ya muda
mrefu.
Profesa Ndulu alisema BoT itahakikisha inaziwezesha benki
kuendelea na jukumu lao la kutoa mikopo pia kuwa wabunifu wa kutafuta
pesa kwa ajli ya amana badala ya kutegemea Serikali pekee.
“Benki
zinaweza kukusanya amana kwa kiwango kikubwa lakini kama nilivyosema
jana (juzi) kuwa katika kila Sh60 kati ya Sh100 zipo kwenye mikono ya
watu badala ya kuwekwa akiba benki hivyo ni muhimu zikawekwa mbinu ya
kuzipata kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji kuzitumia kwenye
uzalishaji,” alisema.
Alisema katika kufanikisha mpango huo
lazima kuvutia mitaji kutoka nje kwani hakuna nchi yoyote duniani
inayoweza kupiga hatua kwa kutegemea fedha za maendeleo na uwekezaji
zitokane na mapato ya ndani pekee akitolea mfano wa China kuwa ni mfano
uchumi wake kutegemea mitaji inayotoka nje ya nchi hiyo.
Katika
hatua nyingine Profesa Ndulu alisema amekubaliana na wadau wa sekta ya
fedha kuongeza nguvu katika kutoa mikopo na kuboresha mifumo ya taarifa
kwa wale wanaotaka mikopo kwa ajili ya kilimo katika mnyororo mzima wa
thamani kuanzia uzalishaji hadi kufika kwenye soko.
Profesa
Ndulu alisema Tanzania imekaa vizuri kijiografia kufanya biashara na
nchi zisizo na bahari zikiwemo Malawi, Uganda, DRC na Zambia katika
kuwezesha sekta ya fedha kusaidia eneo la usafirishaji, bandari kufanya
kazi na huduma kutolewa inavyotakiwa.
Mwenyekiti wa wenye
mabenki ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei
amesema waendeshaji wa mabenki wamenufaika na kuelewa mikakati na fursa
za Serikali ambayo itawawezesha wao kutoa fedha kwa wafanyabishara.
Alisema
wao kama CRDB wameweza kukusanya amana za Sh500 bilioni zinazokopeshwa
kwa wafanyabiashara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na
kufungua matawi madogo madogo 100 nchi nzima.
Dk Kimei alisema
serikali inapobanwa kifedha kutokana na kutegemea mashirika ya umma
inawapa fursa sekta binafsi kupanua wigo wao kuwafikia wananchi wengi.