WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Bw. Bakari Mohammed kuhakikisha hospitali ya wilaya hiyo inakusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Ametoa agizo hilo jana Jumapili, Oktoba 16, 2016 wakati alipotembelea hospitali ya wilaya ya Nachingwea akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amesema Serikali ilishaagiza taasisi zote za umma kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato kwa lengo la kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Amesema taasisi ambazo tayari ziameanza kutumia mfuko huo katika ukusanyaji wa mapato zimeweza kuongeza kiwango cha makusanyo kutoka sh. 300,000 hadi milioni nne kwa siku.
Pia aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambao utawawezesha kupata huduma ya matibabu bure katika kipindi cha mwaka mzima.
Akizungumzia kuhusu matibabu kwa wazee, Waziri Mkuu amemuagiza Bw. Mohammed kuhakikisha anafungua dirisha la kuwahudumia wazee ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma wanapofika hospitalini hapo.
“Mkurugenzi hakikisha watendaji wako wa kata na vijiji wamebaini wazee wote katika maeneo yao na kuwatengenezea vitambulisho vitakavyowawezesha kupatibiwa bure,” amesema.
Naye Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Samwel Laizer amesema muamko mdogo wa jamii kujiunga na CHF ni moja kati ya changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma za afya.
Dk. Laizer amasema kati ya kaya 30,000 zilizoko wilayani Nachingwea ni kaya 7,133 tu ndizo zilizojiunga na mfuko wa CHF.
Awali Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa wilaya hiyo kwenye ukumbi wa Chuo Cha Walimu na kuwataka wabadilike ili waweze kuwatumikia wananchi kwa uadilifu bila ya kujali itikadi zao za kidini na kisiasa.
Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi. “Serikali haitaridhika kuona wananchi wakizagaa kwenye ofisi za halmashauri hiyo bila ya kusikilizwa,” amesema.