MZUNGUKO wa fedha katika uchumi wa Tanzania, umeporomoka kwa kasi katika kipindi kifupi tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano na kuathiri ukuaji uchumi karibu katika kila sekta.
Ripoti ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyotolewa hivi karibuni, ilieleza kuwa mzunguko huo wa fedha, ambao huchangia kujenga uwezo wa ununuzi katika uchumi, umefikia kiwango ambacho hakijawahi kutokea tangu mwaka 2012.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Desemba mwaka jana, mzunguko huo kwa maana ya noti na sarafu mikononi mwa watu na kwenye akaunti za watu benki, ulikuwa asilimia 18.8 lakini uliporomoka na kufikia asilimia 6.7 Julai.
Hali hiyo ilitajwa na ripoti hiyo ya Agosti, kuwa imechangiwa pamoja na mambo mengine, na hatua ya benki za biashara kupunguza utoaji mikopo kwa karibu kila sekta muhimu ya uchumi, kutokana na sekta hizo kushindwa kurejesha mikopo.
Sekta zilizoathirika
BoT imekiri kuwa utoaji mikopo katika sekta binafsi ambayo ndiyo injini ya uchumi, umeshuka kutoka asilimia 23.5 Julai mwaka jana hadi asilimia 15.2 Julai mwaka huu.
Hali mbaya zaidi kwa mujibu wa ripoti hiyo, imeonekana katika sekta za ujenzi, uzalishaji viwandani na hoteli na migahawa.
Katika ujenzi, BoT ilionesha kuwa Julai mwaka jana mikopo iliyotolewa kwenda sekta hiyo ilikuwa asilimia 22.9 ya mikopo yote, lakini Julai sekta hiyo iliambulia chini ya asilimia sifuri ya mikopo yote kwa kupata asilimia -4.
Sekta ya uzalishaji viwandani, BoT ilieleza kuwa mikopo imeshuka kutoka asilimia 30.7 Julai mwaka jana hadi chini ya asilimia sifuri, yaani asilimia -0.7 Julai mwaka huu; huku sekta ya hoteli na migahahawa utoaji mikopo ukitoka asilimia 13.6 Julai mwaka jana mpaka asilimia -0.4 Julai mwaka huu.
Hali ya 2012
Pamoja na kuwa kuporomoka kwa mzunguko wa fedha mwaka huu kumewahi kutokea mwaka 2012, lakini ripoti ya BoT ya Desemba mwaka huo, ilionesha kuwa utoaji mikopo katika sekta muhimu za uchumi, haukuathirika kama ilivyoathirika mwaka huu.
Wakati kuporomoka kwa mzunguko wa fedha mwaka huu kumesababisha utoaji mikopo sekta ya ujenzi kushuka kutoka asilimia 22.9 Julai mwaka jana mpaka chini ya asilimia sifuri, yaani asilimia -4.5 mwaka huu; mwaka 2012 utoaji mikopo katika sekta hiyo haukuyumba kwani ulitoka asilimia 4.4 Novemba 2011 mpaka 4.6 Novemba 2012.
Hali hiyo ya kutoyumba kwa utoaji wa mikopo katika uchumi mwaka 2012, ilijionesha hata katika sekta zingine za biashara, kilimo, viwanda, usafirishaji na hoteli na migahawa; tofauti na utoaji huo wa mikopo mwaka huu, ambapo sekta hizo muhimu zimeyumba kama inavyoonesha katika majedwali ya BoT ya ripoti ya kila mwezi ya Desemba 2012 na ya Agosti.