test

Jumapili, 16 Oktoba 2016

Sintofahamu yaibuka mtihani darasa la 2


MKANGANYIKO umeibuka kuhusu kuwepo au kutokuwepo kwa mtihani wa taifa wa darasa la pili.
Wakati wapo baadhi ya wazazi wanaosema wamejulishwa kuwepo kwa mtihani huo, wengine wanasema wamepokea barua kutoka katika shule wanazosoma watoto wao kuhusu kuahirishwa kwake.

Hata hivyo,hivi karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema mtihani huo haupo kabisa.
Utata huo umeibua mkanganyiko kwa wazazi wengi, ambao watoto wao wanasoma katika shule mbalimbali za msingi nchini kutokana na kuwepo kwa shule ambazo uongozi wake, ulishatoa taarifa kwa wazazi juu ya kuwepo kwa mtihani huo, unaotolewa ili kupima uwezo wa wanafunzi kwenye KKK yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
Wakizungumza na gazeti hilo kwa nyakati tofauti Dar es Salaam, baadhi ya wazazi walisema wamepokea barua inayowaeleza uwepo wa mtihani huo wa taifa, utakaofanyika Novemba 17 na 18, mwaka huu kwa lengo la kupima uelewa wa KKK.
“Nina barua nyumbani tulipewa shuleni kwa mwanangu anasoma Atlas School, barua inazungumzia mambo mengi pamoja na hilo la mtihani wa taifa wa darasa la pili na kwamba katika kutimiza hilo, wanafunzi wamepewa mtihani wa majaribio na wameufanya Oktoba 11 hadi 13, mwaka huu,” alisema mzazi mmoja.
Alisema mwanawe huyo anayesoma darasa la pili, hivi sasa anajiandaa na mtihani huo na wazazi wanafahamu kuwa mtihani huo upo kwa sababu walitangaziwa na shule.
Alisema, hata hivyo, hivi sasa wanafunzi wa darasa la kwanza na pili shuleni hapo, wanasoma masomo saba ambayo ni Kiswahili, Kuandika, Kusoma, Kuhesabu, Sayansi, Stadi za Kazi, Haiba na Michezo, hatua inayozidisha mkanganyiko.
Wakati mzazi huyo akisema hayo, mzazi mwingine ambaye mtoto wake anasoma darasa la pili katika Shule ya Msingi Tusiime, alisema awali wazazi walitaarifiwa kuhusu uwepo wa mtihani huo; na wanafunzi walianza kujaza fomu, lakini baadaye waliambiwa haupo.
‘’Nakumbuka shuleni kwa mwanangu waliambiwa kuhusu mtihani huo wa darasa la pili, na walianza kujaza fomu, ila baadaye wakaambiwa haupo, hatujui utafanywa lini,” alisema.
Mzazi mwingine ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Mountain Hill jijini Dar es Salaam, alisema katika kikao cha wazazi cha Septemba, mwaka huu wazazi waliambiwa kuwa mtihani huo wa taifa kwa darasa la pili, umeahirishwa hadi mwakani.
“Nilienda kwenye kikao cha wazazi cha Septemba shuleni Mountain Hill na mwanangu anasoma darasa la pili, tuliambiwa mtihani wa darasa la pili wa taifa wa KKK haupo, bali utafanywa mwakani,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Ndalichako alisema serikali haijawahi kuwa na mtihani wa darasa la pili; na kwamba watoto hao bado ni wadogo, hivyo hawastahili kupewa mtihani.
“Mtihani wa darasa la pili hatujawahi kuwa nao, halafu hawa watoto wadogo unaanza kuwapa mtihani, ni wadogo,” alisema Profesa Ndalichako, hatua ambayo inazidisha sintofahamu kwa suala hilo.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx