Vitendo
vya ukatilitili wa kijinsia kwa watoto vimeendelea kuongezeka kwa kasi
nchini katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai mwaka huu ambapo
zaidi ya watoto 2,570 wa kike na kiume wamelawitiwa na kubakwa.
Akizungumza
katika sherehe za maadhimisho ya miaka 21 ya Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC) yaliyofanyika jana katika Makao makuu ya watoto
yaliyopo Kurasini jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC
Helen Kijo-Bisimba alisema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na ya mwaka
jana.
Hata
hivyo, Mama Bisimba alisema kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi,
takwimu hizo zinaweza kuwa ndogo kutokana na kesi nyingi za ubakaji na
ulawiti kwa watoto kutoripotiwa polisi kwa sababu ya mila na desturi za
maeneo mengi nchini.
“Ripoti
ya Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia kati ya Januari na Machi
2016 inaonyesha matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa yakiendelea
kuongezeka kutoka 180 hadi 1765 hayo ni matukio yaliyotolewa taarifa
katika vituo mbalimbali vya polisi nchi nzima ukilinganisha na matukio
1585 mwaka 2015. Hata hivyo waliohusika na matukio hayo wameonekana
wakirandaranda bila kuchukuliwa hatua za kisheria, ” alisema.
Alisema
ripoti hiyo inaonyesha kuwa kesi 1,203 zipo katika hatua ya upelelezi,
822 zipo mahakamani na watuhumiwa 234 wamekwisha hukumiwa.
“Pia
utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto
kwa kushirikiana na Tanzania kitengo cha ustawi wa jamii unaonyesha kati
ya watoto 10 wa kike 4 wamebakwa, na kati ya watoto 10 wa kiume 3
wamelawitiwa zaidi ya mara tatu. Utafiti huo unaonyesha kwa ujumla kuwa
watoto wa kike na wa kiume 6 walifanyiwa ukatili huo na watu ndani ya
familia,” alisema.
Bisimba
alisema asilimia 49 ya ukatili hufanyika nyumbani, 23 hufanyika njiani
wakati wa kwenda shule au kurudi, na asilimia 15 hufanyika shuleni. Pia
ripoti hiyo ya UNICEF inaonyeaha kuwepo kwa matukio ya watoto
kulawitiana na kubakana wenyewe kwa wenyewe kutokana na kuvizoea vitendo
hivyo.
LHRC
imeitaka serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kuifanyia
marekebisho sheria ya mtoto na kutilia mkazo malezi bora kwa watoto
ikiwemo kuweka kipengele kitakachotoa adhabu kali kwa familia
itakayoshindwa kutoa malezi bora kwa mtoto.
LHRC inayoshughulika na utetezi wa sheria na haki za binadamu ilianzishwa Septemba 26, 1995.