WAZIRI
MKUUkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wiki moja kwa Afisa Elimu Mkoa wa
Pwani, Yussuph Kipengele kupeleka walimu wa kufundisha masomo ya kidato
cha tano na sita katika shule za sekondari za Mkongo na Utete wilayani
Rufiji.
Ametoa
agizo hilo Jumatatu, Septemba 26, 2016 wakati akizungumza na wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Jumba la
Maendeleo wilayani Rufiji. baada ya Mbunge wa Rufiji, Muhammed
Mchengelwa kumwambia kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya
ukosefu wa walimu wa kidato cha tano na sita licha ya kuwa na shule.
"Hatuwezi
kuwa na shule ambazo hazina walimu, nasikia hapa anayefundisha ni Mkuu
wa shule na mwalimu mmoja tu, wakati kule Kibaha kuna walimu
walmerundikana ,sasa fanya realocation tarehe 4,Oktoba uniletee taarifa
walimu wamefika Rufiji.",alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia
suala la upungufu wa watumishi wa umma kwenye sekta mbalimbali, Waziri
Mkuu alisema baada ya kazi ya uhakiki watumishi hewa itakapokamilika,
serikali itaangalia kwenye maeneo yenye upungufu na hivyo kutangaza
ajira.
"Hivi
sasa serikali inakamilisha masuala ya uhakiki wa watumishi,
tukimakamilisha na kujua idadi ya watumishi na maeneo yenye upungufu
tutaanza tena kuajiri, tulisitisha kupisha kwanza kazi hii,alisema
Waziri Majaliwa.
Kuhusu
migogoro ya wakulima na wafugaji Waziri, Mkuu alisema watendaji wa
halmashauri na vijiji wanapaswa kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima
na kutaka mifugo isiongezwe kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwa.
Alisema
wenyeviti wa vijiji wanapaswa kusimamia utekelezaji wake katika mpango
wa matumizi bora ya ardhi na kwamba atakayeruhusu idadi kubwa ya mifugo
kuingia kijijini zaidi ya ile iliyokubalika atawajibishwa ikiwemo
kufukuzwa kazi na hatua nyingine za kisheria.
"Hatuwezi
kuendelea kuwa na watumishi wasio na nidhamu, wale wote watakaoingia
mifugo zaidi ya uwezo wa kijiji wafukuzwe kazi na kuchukuliwa hatua,
lakini pia wafugaji ni marufuko kuingiza mifugo kwenye mazao ya
wakulima"alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu
ujenzi wa barabara ya lami kwenda makao makuu ya wilaya ya Rufiji,
Utete, Waziri Mkuu aliahidi kuchukua ombi hilo na kusema bajeti ijayo
litatengewa fedha kuwa ajili ya kufanya maandalizi ya upembuzi kuona
gharama yake kabla ya kutangaza zabuni ya ujenzi.
Kuhusu
utengenezaji wa madawati, Waziri Mkuu alisema ifikapo Oktoba 30, mwaka
huu kila wilaya nchini inapaswa iwe imekamilisha utengenezaji wa
madawati hayo kwenye shule nchini.
Aidha,
alisema ipo miradi mingi inayoendeshwa kwa maslahi binafsi ukiwemo
mradi wa Bonde la Rufiji(RUBADA), ambao wamebaini kuna ubabaishaji
mkubwa, hivyo wamepeleka timu ya wataalamu kuhakiki ili wale wabadhirifu
wachukuliwe hatua.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 26, 2016