SEP 15, 2016
NAHODHA wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya FC Genk ya Ubelgiji ameonesha masikitiko yake kwa tukio la tetemeko la ardhi lililotokea Bukoba mwishoni mwa wiki iliyopita.
NAHODHA wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya FC Genk ya Ubelgiji ameonesha masikitiko yake kwa tukio la tetemeko la ardhi lililotokea Bukoba mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mwishoni mwa wiki iliyopita mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi saa 9:27 alasiri.
Nguvu ya mtetemo wa tetemeko hilo ilikuwa ni 5.7 kwa kutumia kipimo cha ‘Ritcher’ ukubwa ambao ni wa juu kiasi cha kuleta madhara makubwa ikiwamo kuvunjika nyumba, kujeruhi na watu 17 kupoteza maisha.
Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Samatta aliandika: “Poleni wakazi wa Bukoba, kwa kupoteza ndugu pamoja na mali kutokana na tetemeko la ardhi, Mungu awatie nguvu na pia tuwaombee waliotangulia”.
Samatta kabla ya kujiunga na Genk alikuwa mchezaji wa TP Mazembe ya Congo DR, ambako alicheza kwa mafanikio na kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika kwa wcahezaji wa ndani mwaka jana.
Mbali na Samatta, mwanasoka mwingine aliyeguswa na tetemeko hilo na kutoa salamu za pole ni Mkenya Victor Wanyama anayecheza soka ya kulipwa katika timu ya Tottenham ya England.
Wanyama aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter: “Hisia na maombi yangu ni kwa watu wa Tanzania na Bukoba kufuatia tetemeko la ardhi Tuko Pamoja”. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema baada ya kamati ya maafa ya mkoa na kamati ya maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wamefanya tathmini ya haraka na kubaini mahitaji kwa waathirika.
Kijuu alitaja baadhi ya mahitaji muhimu yanayohitajika kwa waathirika wa tukio hilo ni vifaa vya ujenzi mabati 90,000 yenye gharama ya Sh bilioni 1.7, saruji yenye thamani ya Sh milioni 162, mbao zenye thamani ya Sh milioni 450 na misumari yenye thamani ya Sh milioni 12 ambapo jumla ya fedha zinazohitajika ni Sh bilioni 2.3.
Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi alihamasisha wafanyabiashara na mabalozi ambao walichangia Sh bilioni 1.4.

