Uingereza
imetoa mchango wa Shilingi Bilioni 6 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili
ya kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule zilizopata madhara kufuatia
tetemeko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera tarehe 10 Septemba,
2016.
Mchango
wa fedha hizo umewasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah
Catherine Cooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Balozi
huyo kuwasilisha hati zake za utambulisho.
Balozi
Sarah Catherine Cooke amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kutoa
mchango wa fedha hizo Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May anatoa
pole kwa Serikali ya Tanzania na kwa familia zote zilizopatwa na madhara
ya tetemeko hilo na kwamba Uingereza imeona ishirikiane na Tanzania
katika kukabiliana na madhara hayo.
“Uingereza
imeguswa sana na maafa yaliyowakumba wananchi kufuatia tetemeko
lililotokea Kagera, tunapenda kuona wananchi wanasaidiwa na wanafunzi
wanaendelea na masomo” amesema Balozi Sarah Catherine Cooke.
Kwa
Upande wake Rais Magufuli amemshukuru Waziri Mkuu wa Uingereza kwa
mchango huo ambao utasaidia juhudi za Serikali za kuhakikisha inarejesha
miundombinu iliyoharibika zikiwemo shule.
“Mhe.
Balozi Sarah Catherine Cooke naomba unifikishie shukrani zangu za dhati
kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May na umueleze kuwa kwa
niaba ya watanzania hususani waliopatwa na madhara ya tetemeko la ardhi
tumeguswa sana na moyo wake wa upendo kwetu” amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli na Balozi Sarah Catherine Cooke pia wamezungumzia uhusiano na
ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza ambapo Rais
Magufuli ametoa wito kwa Balozi huyo kuendelea kuwahamasisha
wafanyabiashara na wawekezaji wa Uingereza kuongeza uwekezaji wao hapa
nchini na kwamba Tanzania itaendeleza na kukuza uhusiano huo.
“Uingereza
ni rafiki na ndugu wa kweli na wa kihistoria kwa Tanzania, tunatambua
kuwa nchi yenu ni mdau mkubwa na muhimu wa maendeleo yetu, hivyo
tusingependa kupoteza rafiki na ndugu yetu, tuendelee kushirikiana kwa
manufaa ya wananchi.
“Natambua kuwa Uingereza ina utaalamu mkubwa katika masuala ya gesi hivyo nawakaribisha waje wawekeze katika sekta ya gesi” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli amesema Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kwa
ajili ya kusaidia kukabiliana na madhara ya maafa ya tetemeko la ardhi
lililotokea mkoani Kagera zinafikishwa kwa walengwa na ameonya kuwa
watakaothubutu kuiba fedha hizo watashughulikiwa.
Dkt.
Magufuli amebainisha kuwa baada ya kutengua uteuzi na kuchukua hatua
nyingine dhidi ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Amantius
Msole na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Bw. Steven Makonda pamoja na
kumsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw. Simbaufoo Swai,
amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei
awachukulie hatua watumishi wa Benki hiyo walioshirikiana na watumishi
hao kufanya njama za kuanzisha akaunti nyingine ya benki yenye jina
linalofanana na akaunti rasmi ya “Kamati ya Maafa Kagera” kwa lengo la
kujipatia fedha”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Septemba, 2016