JESHI la Polisi nchini limeondoa katazo la mikutano ya ndani kwa vyama vya siasa kuanzia jana.
Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni takribani mwezi mmoja tu tangu Jeshi hilo kupitia kwa Kamishna wake wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya, lilipotangaza kuzuia mikutano yote ya ndani ya vyama vya siasa nchini.
Kamishna Mssanzya alitangaza kuondoa zuio hilo jana na kusema kuwa makatazo mengine ya mikutano ya vyama hivyo, yako pale pale.
“Kuanzia leo Jeshi la Polisi linaondoa katazo lake la mikutano ya ndani ya vyama vya siasa na linasisitiza kuwa maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, bado imezuiliwa, isipokuwa ya wabunge katika majimbo yao,” alisema Mssanzya.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi, limekuwa likifuatilia hali ya usalama hasa inayohusiana na shughuli ya vyama vya siasa na sasa Jeshi la Polisi limejiridhisha kwamba kumekuwepo na hali ya kuridhisha kiusalama, hivyo kuona hakuna haja kiusalama kuendelea kuzuia mikutano ya ndani.
Hatua ya kuzuia mikutano ya ndani ya vyama vya siasa nchini, ilitokana na baadhi ya vyama vya siasa kutumia mikutano hiyo ya ndani, kuendeleza ajenda za kuchochea wananchi kutokutii sheria za nchi, kupandikiza wananchi chuki dhidi ya serikali yao na kuhatarisha hali ya usalama kwa ujumla wake.
Mssanzya alisema Jeshi la Polisi, halitasita kuchukua hatua kwa mtu au kundi la watu litakaloenda kinyume na sheria na halitasita kurejesha zuio hilo tena, endapo vyama vitaendeleza masuala ya uchochezi.
Alisema bado wanaendelea na uchunguzi, hivyo endapo kama watabaini kuimarika kwa amani na utulivu, wataondoa pia zuio la mikutano ya hadhara na maandamano.
Aidha Jeshi la Polisi liliwataka wananchi na vyama vya siasa, kuheshimu sheria za nchi na wakati wote kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, amesema, Polisi haikuwa na mamlaka ya kuzuia mikutano hiyo hapo awali, na wao walikuwa wakiendelea kuifanya.
“Polisi haina mamlaka ya kuzuia wala kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano yake, iwe ya ndani au ile ya hadhara, na kilichofanyika ni ukiukwaji tu wa sheria,” alisema Makene.
Aidha, Makene alisema kuwa leo itafanya mkutano na vyombo vya habari, kutolea ufafanuzi taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi.