Mkuu
wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameliagiza jeshi la polisi mkoa
wa Dar es salaam kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwepo kitu
kinaitwa UKUTA ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.
Akizungumza jana na kikosi cha kutuliza ghasia katika kambi ya Ukonga Jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa alisema kwa kuwa askari wanafahamu sheria wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo au maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaagiza kinachotakiwa ni utekelezaji.
‘’Msisubiri maelekezo yoyote kutoka juu, asiwepo mtu yeyote akafunga
duka kwa sababu ya UKUTA, nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza
kusimama mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini hatutakuwa na
vurugu kwenye Mkoa wetu na hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua
madhara ya vurugu’’ Alisema Makonda.
Aidha
kwa upande wake Kamanda wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas Mkondya alisema
jeshi la polisi lipo vizuri na vijana wameandaliwa vizuri na
wameandaliwa kuwa tayari siku nyingi na hakuna mtu yeyote atakayethubutu
kufanya UKUTA na watakaofanya hivyo watazimwa kabla hawajafanya
chochote.
Kamada aliwataka
wananchi wote Jijini Dar es Salaam kuto jitokeza kwenye oparesheni
UKUTA kwa kuwa maandamano hayo siyo halali na watakaojitokeza watapata
matatizo yasiyowahusu.
Oparesheni
UKUTA ilitangazwa na CHADEMA ikiwa na maana Umoja wa Kupinga Udikteta
Tanzania na ikatajwa tarehe Mosi Septemba nchi nzima chama hicho
kitafanya mikutano ya hadhara jambo ambalo limepingwa na serikali
kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufuatia wakuu wa
mikoa.