SERIKALI
imesema haina ushahidi wa kutosha kuzitia hatiani shule za Feza nchini
zinazodaiwa kumilikiwa na mmoja wa wananchi wa Uturuki anayetuhumiwa
kujihusisha na ugaidi na kuitaka Serikali ya Uturuki kuwasilisha taarifa
zenye ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma hizo.
Kauli
hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga.
Alisema
walipokea madai kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini kuwa shule hizo
zinamilikiwa na mmoja wa wananchi wa nchi hiyo anayejihusisha na ugaidi.
Balozi
Mahiga alisema katika madai ya ubalozi huo, shule hizo ni miongoni mwa
miradi inayomilikiwa na mtuhumiwa huyo na kwamba, baadhi ya walimu wake
hutumia mbinu za kigaidi kufundisha wanafunzi.
Akijibu
tuhuma hizo, Balozi Mahiga alisema serikali kabla ya kutoa kibali kwa
mwekezaji au mfanyabiashara yeyote kuendesha shughuli zake nchini,
vyombo vya usalama nchini, hufanya upelelezi wa kina na wamejiridhisha
kwamba wafanyabiashara wa Uturuki waliopo nchini wanafanya biashara
halali.
“Ni
kweli tumepokea tuhuma kutoka kwa Ubalozi wa Uturuki nchini kuhusu
shule za Feza kwamba ni sehemu ya makundi ya kigaidi, lakini hatuwezi
kuzitia hatiani shule hizo hadi tuletewe ushahidi wa kutosha,” alisema Balozi Mahiga.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya
Shule za Feza, Habib Miradji alisema shule hizo ni za asasi
iliyosajiliwa kisheria na Serikali ya Tanzania hivyo ni mali ya Tanzania
na endapo kuna kitu au tatizo ni lazima wawasiliane na serikali na
watafika kukagua ili kama kuna lolote baya hatua zichukuliwe.
Aidha alisema kwamba shule hazijafungwa.