Utunzi
mahiri wa mashairi na ughani uliotukuka wa Mrisho Mpoto, umeligusa
sikio la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli ambaye ameeleza kuwa shabiki mkubwa wa kazi za msanii huyo
hususan wimbo wake ‘Sizonje’.
Akizungumza
na Mpoto jana, muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais Magufuli
alimueleza msanii huyo kuwa anazifahamu vizuri kazi zake na kwamba
anaupenda sana wimbo wake wa ‘Sizonje’ huku akichambua baadhi ya mistari
iliyomo kwenye beti za wimbo huo.
Mpoto
alikuwa msanii pekee aliyeongozana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye, Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Wakuu wote wa Wilaya za Dar es Saalam
pamoja na viongozi wengine waliofika katika uwanja huo wa ndege kumpokea
Mkuu huyo wa nchi.
“Nasikiliza
sana nyimbo zako, ila huu wimbo wako wa Sizonje nimeuelewa sana na
nausikiliza kila siku, kwangu umekuwa kama wimbo wa taifa. Mwanzoni
nilipata tabu kuuelewa lakini sasa hivi… aaaah, nimeuelewa vizuri sana.
Halafu Sizonje namjua, nimtaje?,” yalisikika baadhi ya maneno ya Rais Magufuli kwa Mrisho Mpoto.
Akielezea
tukio hilo lililoleta msisimko wa aina yake uwanjani hapo, Mpoto
alisema kuwa baada ya kumsikia Rais ameanza kuusifia wimbo wake
alishtuka na kujawa na furaha ya aina yake kwani kwa msanii ni jambo la
thamani kubwa kusifiwa kazi yake na Mkuu wa Nchi.
Alisema
kuwa pamoja na kuusifia wimbo huo, Rais alionesha kuufahamu vizuri
zaidi baada ya kuanza kuipitia baadhi ya mistari na kuahidi kumfumbulia
fumbo lililofichwa kwenye wimbo huo watakapokutana tena.
“Unapopata thamani kutoka kwa Mkuu wa Nchi inaleta faraja sana," amesema Mpoto.
"Kwahiyo, mheshimiwa Rais leo kuniambia kwamba yeye ni shabiki wa kazi
zangu na kwamba anapenda sana wimbo wa Sizonje, na akafunguka kwa
mistari ‘minane’ ya Sizonje ikiwa ni pamoja na ile inayosema ‘huyu mgeni
anayepitia madirishani wakati milango ipo!’ Na akaniambia siku
tukikutana ataniambia vile vyumba vitatu kwanini havifunguki,” aliongeza.
Msanii
huyo amemshukuru Rais Magufuli kwa kuthamini mchango wake katika sanaa
kwakuwa anaamini kuthaminiwa ni hitaji kubwa la kila msanii.
“Kwakweli
leo ni siku yenye furaha sana. Najisikia furaha sana. Asante sana
mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. Umenifanya nimekuwa na siku nzuri
sana,” Mpoto alifunguka kwa furaha.
Mwaka
huu mwanzoni, Mrisho Mpoto aliachia audio na video ya ‘Sizonje’
aliomshirikisha Banana Zorro ambapo kwa muda mfupi tu, wimbo huo
uligeuka kuwa mkubwa na kufanya vizuri. Kutokana na ufanisi wa kazi
zake, Mpoto ameendelea kukubalika akipata mikataba ya ubalozi wa
mashirika na taasisi kubwa nchini ikiwa ni pamoja na mfuko wa pensheni
wa PSPF.
Mpoto
ambaye mwaka jana alipewa tuzo ya heshima ya WASTA ya nchini Kenya
kutokana na mchango wake katika lugha ya Kiswahili, amejipatia heshima
kubwa kutokana na utunzi mahiri wa nyimbo za awali, zikiwemo Nikipata
Nauli, Adela, Chocheeni Kuni, Samahani Wanangu, Waite, Njoo Uichukue na
zingine.