Wataalamu
wa Tanzania na Afrika Kusini wapo katika mkutano wa siku nne wa kuandaa
mpango bora wa kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali kwa madhumuni ya
kukuza uchumi wa nchi hizo.
Mkutano
huo unaojulikana kama Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National
Commission-BNC) umefunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima jijini
Dar Es Salaam leo.
“Mkutano
huu ni muhimu sana kwa kuwa licha ya nchi zetu kuwa na uhusiano na
ushirikiano mzuri tokea enzi za ubaguzi wa rangi, lakini bado utakuwa
chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii
katika maeneo tutakayokubaliana na wenzetu” Balozi Mlima alisema.
Balozi
Mlima alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha
Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential Economic Commission-PEC) mwaka
2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini BNC ambayo ilichukuwa nafasi ya
PEC. Tokea uwekaji saini wa makubaliano hayo, chombo hicho hakikuweza
kukutana licha ya kuwa, makubaliano hayo ndiyo yatakuwa mwongozo katika
majadiliano yatakayoendelea hadi tarehe 11 Mei 2017.
Kwa
mujibu wa Balozi Mlima, uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Afrika
Kusini unaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda. Kwa takwimu
zilizopo takribani makampuni 226 ya Afrika Kusini yamewekeza nchini
mtaji wa jumla ya Dola za Marekani milioni 803.15 na kuajiri zaidi ya
watu 20,917. Alisema idadi ya makampuni inaweza kuongezeka kwani kuna
makampuni mengi mapya kutoka Afrika Kusini yameshaonesha dhamira ya
kuwekeza nchini.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya
Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Bw. Edward Makaya alieleza kuwa Tanzania
na Afrika Kusini hazijafanya vya kutosha kwenye ushirikiano wa kiuchumi
na kijamii. Alisema hadi wakati huu nchi hizo zimesaini makubaliano na
mikataba takribani 14 ambayo ni michache ukilinganisha na urafiki na
udugu uliopo baina ya nchi hizo.
Hivyo,
alisistiza umuhimu wa kikao hicho kufanya majadiliano yatakayowezesha
uwekaji saini wa mikataba mingi zaidi. Alisisitiza umuhimu wa mikataba
hiyo kuzingatia maslahi ya pande zote.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 08 Mei, 2017