MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amesisitiza kutekelezwa kwa mpango wa serikali kuhamishia makazo yake mkoani Dodoma ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utawala wake huku akitangaza kuigeuza Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam kuwa sehemu ya maonyesho.
Aidha,
Rais Magufuli amesema majengo ya wizara mbalimbali yaliyopo karibu na
mwambao wa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam yatauzwa kwa wawekezaji
mbalimbali ili yageuzwe hoteli za kitalii na fedha zitakazopatikana
zitatumika kuustawisha mji wa Dodoma ambako serikali inahamia.
Magufuli
alitangaza mpango huo jana wakati akizungumza na viongozi na wanachama
wa chama hicho muda mfupi baada ya kutembelea ofisi yake ya kichama
iliyopo ndani ya jengo la Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba
jijini Dar es Salaam.
Rais
Magufuli alisema wale wanaosema kuwa amesema atauza Ikulu baada ya
kuhamia Dodoma wanapotosha ukweli kwa sababu serikali haina mpango huo.
“Wengine
wanasema Ikulu itauzwa.. jengo la Ikulu litabaki pale, litakuwa jengo
la maonyesho… wizara na majengo mengine yaliyo jirani na bahari yatauzwa
ili tupate fedha za kuiendeleza Dodoma,” alisema Magufuli.
Alisema
Serikali inahamia Dodoma ili Dar es Salaam ipumue na ili viongozi
wakitaka kuja waje kwa ajili ya kutembea lakini shughuli zote za
Serikali zitakuwa zimehamia mkoani humo.
Aidha,
Rais Magufuli aliwashangaa watu wanaokejeli mpango wake wa kuhamishia
Serikali Dodoma na kubeza kwa kudai kuwa haiwezekani.
“Suala
la kuhamia Dodoma limeanza tangu mwaka 1973. Nimesoma darasa la kwanza
hadi Chuo Kikuu, nikamaliza bado hatujahamia… hatuwezi kujenga Serikali
kwa mchakato, mchakato umekwisha, nimesema ndani ya miaka minne na miezi
minne iliyobaki, nitahikikisha tutakuwa tumeshaondoka Dar es Salaam,” alisisitiza.
Alishangaa
pia watu wanaohoji kwamba watapata wapi makazi iwapo Serikali itahamia
mkoani humo na kuhoji kuwa mbona wakati wa Bunge watumishi hao hao huwa
wanakwenda kwa wingi na wanapata makazi.
“Wakati
wa Bunge, zaidi ya watu 300 huwa Dodoma, mawaziri, manaibu na makatibu
wakuu, wanakaa na wanatosha… kwa nini hili wanahoji watakaa wapi,” alisema.
“Nazifahamu
ofisi zote ukitoka Hoteli ya Kilimanjaro mbele kuna ofisi ya Takwimu,
Wizara Ardhi, Utumishi zote zimetazama baharini… tutatangaza zabuni watu
wanaotaka kujenga hoteli watanunua huko kote kuwe eneo la kitalii,
tukipata fedha tutaweka makandarasi kujenga Dodoma. Hakuna
kinachoshindikana, kinashindikana kwenye akili zetu,” alisema.
Aidha,
alisema awali wakati wakitangaza kwenda Dodoma, kulikuwa hakuna
miundombinu, maji, umeme wala barabara lakini sasa kila kitu kipo na
mipango ya kuiboresha Dodoma ipo.
Alisema Dodoma ikijengwa miji mingine itakuwa na utalii utaongezeka kwa sababu huo (Dodoma) ni mji ambao upo katikati ya nchi.
“Kutoka
Dodoma kwenda Arusha ni saa moja na nusu na maeneo mengine hii
itasaidia watu wa mikoa mbalimbali kuja kuwekeza Dodoma na wamachinga
nao watakuja,” alisema.