Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa amewaasa watanzania kuacha kufuata mkumbo wa kisiasa badala yake watii mamlaka ili kuepuka kuvunja sheria na kuleta madhara kwao binafsi na taifa kwa ujumla.
Msekwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala mbalimbali kuhusu mwenendo wa siasa za hapa nchini na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Alieleza kuwa watu wengi wana hulka ya kufuata mkumbo kwenye mambo fulani bila ya kuchunguza na kufahamu ukweli wake kabla ya kushabikia.
“Ni hulka ya watanzania kushabikia mambo wasiyoyafahamu ilimradi tu yanawafurahisha masikioni au machoni mwao kwani hata huko mitaani wanakimbilia ngoma bila ya kujua inatokea wapi au inaelekea wapi, hivyo nawasihi wajaribu kuwa makini na mbinu za siasa zinazotumiwa na baadhi ya vyama kwa kuwa nyingine zina madhara ndani yake.” Alisema Msekwa.
Akifafanua mwenendo wa siasa za hapa nchini, Mzee Msekwa alisema kuwa bado wanasiasa wengi hawafuati kanuni za ushindani wa kisiasa katika kutafuta madaraka badala yake wanatumia mbinu ambazo zinavunja sheria za nchi na hatimaye wanapambana na mamlaka.
“Ushindani wa kisiasa ni jambo la kawaida na linalokubalika ingawa ushindani huo ni lazima ufuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kufikia lengo, hivyo kubuni vitu ambavyo vinachochea utovu wa nidhamu na uvunjifu wa amani sio jambo zuri, ' alisisitiza.
Aidha, Msekwa alieleza kuwa utendaji wa Mhe. John Magufuli ni wa kuridhisha na wa aina yake kwa kuwa amekusudia kuleta mabadiliko chanya kwa watanzania na kuondoa mfumo wa utendaji kazi kwa mazoea jambo ambalo limesaidia kurudisha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.
Akizungumzia uzoefu wake katika masuala ya kuongoza Bunge, alieleza kuwa tofauti ya Bunge la zamani ni kwamba lilikuwa na nidhamu kubwa na linaheshimika lakini Bunge la sasa halina utii na hicho ndio chanzo cha malumbano yanayojitokeza mara kwa mara katika vikao vya Bunge.
Aliongeza kuwa tangu awali wapinzani kazi yao ni kuipinga Serikali iliyo madarakani lakini kwenye Bunge la uongozi wake walikuwa wakipinga kwa kutumia hoja na kufuata kanuni bila ya kudharau mamlaka ya Spika wala Serikali iliyoko madarakani.
“Kanuni zinatoa nafasi kwa mbunge asiyeridhika na maamuzi ya Spika kushitaki kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge, na kamati hiyo itasikiliza na kutoa uamuzi kama mahakama inavyosikiliza lakini wabunge wa sasa hawataki kutumia utaratibu bali hutumia mbinu za tofauti ili waweze kupata sifa ambazo hazina tija kwa wananchi waliowachagua,” alisema.
Msekwa pia amewaasa vyama vya upinzani kutumia mbinu nzuri katika kutafuta madaraka bila ya kuvunja sheria au kuhatarisha amani ya nchi kwani waliowachagua wanategemea zaidi matokeo ya kazi waliyoahidi kuwatumikia kuliko malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wao na taifa.