Lema alikamatwa siku hiyo saa 12 alfajiri akiwa nyumbani kwake, Njiro, na hadi sasa anashikiliwa katika mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Arusha.
Kutokana na kuendelea kugoma kula, Wakili wake, John Mallya amesema leo saa sita mchana atakwenda Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kufungua kesi ya kutaka mteja wake afikishwe mahakamani.
Malya jana alisema katika kesi hiyo atashirikiana na Chadema kuwashtaki mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, Mkoa wa Arusha.
Tangu mbunge huyo akamatwe amegoma kula kwa kile anachodai kupinga udhalilishwaji aliofanyiwa na polisi wakati wa kukamatwa.
Pia, Lema anasema alinyanyaswa mbele ya watoto wake nyumbani kwake huku wakijua yeye ni kiongozi na amechaguliwa na wananchi.
Neema, mkewe Lema,jana alithibitisha kwamba mumewe amegoma kula.
“Anaendelea kugoma kula mpaka sasa kwa sababu hata sasa nimetoka polisi asubuhi kumpelekea chakula, lakini amekataa kula.
“Lakini nilipouliza pale polisi kuwa wanampeleka lini mahakamani, nilijibiwa wanaendelea kumhoji,”alisema Neema.
Juzi, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa alihojiwa dhidi ya matamshi ya uchochezi na kuwa atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika uchunguzi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, Lema anatuhumiwa kuwachochea wakazi wa Arusha kuandamana Septemba mosi, mwaka huu kuhamasisha kile kinachoitwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).