MAMLAKA
ya kugomea dhamana za watuhumiwa aliyokuwa nayo Biswalo Mganga,
Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), sasa imeondolewa na mahakama kuu.
Awali,
DPP alikuwa na uwezo wa kuzuia dhamana za baadhi ya watuhumiwa kwa
namna alivyoona inafaa licha ya kuwepo kwa malalamiko ya uhalali wa
kuzia dhamana hizo......
Miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na DPP ni maslahi ya umma hivyo kusababisha haki ya kupata dhamana kuwa ngumu.
Kwa kuwa hatua hiyo inakiuka Katiba ya Tanzania, Mahakama Kuu imefikia uamuzi wa kumwondolea mamlaka hayo DPP.
Kifungu
kilichokuwa kikimpa mamlaka DPP ya kuzuia dhamana ni 148 (4) cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na kwamba, kinakwenda kinyume na
Ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba ya Tanzania.
Uchambuzi
wa udhaifu wa kifungo hicho kilichokuwa kikitumiwa na DPP ulitolewa na
Majaji Sekieti Kihiyo na Dk. John Ruhangisa wakiongozwa na Jaji Kiongozi
Shaaban Lila.
“Imeamriwa
mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa polisi au mtuhumiwa yoyote,
anatakiwa kupewa haki yake ya kujitetea kabla ya haki hiyo haijazuiliwa
na mkurugenzi wa mashitaka kwa pingamizi la kuwanyima dhamana,” sehemu ya taarifa ya majaji hao imeeleza hivyo.
Kifungu cha 148 (4) kinasema;
“bila kujali kitu chochote kilichopo kwenye kifungu hiki, hakuna afisa
polisi wala mahakama atakayeweza, baada ya mtu kukamatwa na wakati
anasubiri shauri au rufaa, atathibitisha kwa maandishi kwamba kuna
uwezekano kwa usalama au maslahi ya Jamhuri.
“…na
cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka chini ya kifungu hiki
kitaanza kutumika kuanzia terehe kitakapowasilishwa mahakamani au
kutaarifiwa kwa afisa msimamizi wa kituo cha polisi na kitaendelea
kutumika hadi mwenendo utakapohitimishwa ama mkurugenzi wa mashitaka
atakapokiondoa.”
Kuondolewa
kwa mamlaka ya DPP kuzuia dhamana za watuhumiwa kulitokana na kupelekwa
pingamizi la kikatiba lililowasilishwa na Jeremiah Mtosebya, Mkazi wa
Jiji la Dar es Salaam ambaye amesema kifungu hicho kinakiuka Katiba ya
Tanzania.