Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu
wameandikiwa barua na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
wakitakiwa kujieleza kwa matamko yao waliyoyatoa katika siku za hivi
karibuni.
Lissu
amekiri kupokea barua kutoka kwenye Sekretarieti hiyo akieleza kuwa
imeandikwa na Jaji mmoja mstaafu ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
“Ni
kweli mimi na Mwenyekiti Mbowe tumepata barua hiyo. Ni barua ya ajabu
ambayo imeandikwa na mtu aliyewahi kuwa Jaji wa mahakama kuu,” Lissu anakaririwa na Mwananchi. “Sitaki kuzungumza mengi kwa sasa, Jumatano nitalizumzia vizuri jambo hili,” aliongeza.
Hata
hivyo, Kamishna wa Sekretarieti, Jaji Mstaafu Salome Kaganda alieleza
kutofahamu chochote kuhusu barua hiyo iliyodaiwa kuwafikia viongozi hao
wa Chadema.
“Mimi sifahamu kuhusu suala hilo, sina taarifa,” Jaji Kaganda alimueleza mwandishi wa gazeti hilo.
Hata
hivyo, hali hiyo imeibua maswali kwani viongozi hao wa siasa ambao pia
ni wabunge, hawana sifa za kuwa watumishi wa umma na hakuna kiapo cha
utumishi wa umma kinachowabana.
Mbowe
na Lissu walihojiwa hivi karibuni na Jeshi la Polisi kutokana na
matamshi yao wakati wa kutangaza Operesheni UKUTA. Lissu anadaiwa kutoa
kauli za kichochezi na kuidharau mahakama.