Siku moja baada ya kuhukumiwa kulipa faini Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la shambulio la kawaida dhidi ya aliyekuwa mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu uliopita, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuwania tena ubunge katika jimbo hilo.
Mbowe aliyeepuka kwenda jela kwa kulipa
faini hiyo juzi, alitangaza uamuzi huo jana alipokuwa akihutubia mkutano
wa hadhara katika eneo la stendi ya zamani mji mdogo wa Bomang’ombe,
Kilimanjaro.
Mwenyekiti huyo alifikia hatua hiyo
baada ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo kumshinikiza agombee
ubunge na kumchangia Sh800,000 za kuchukua fomu ambayo ndani ya Chadema
hugharimu Sh250,000.
“Nashukuru
kwa walioanzisha wazo hili lakini zaidi ninawashukuru waliojitolea
kunichangia fedha. Nimekubali nitagombea ubunge katika uchaguzi ujao,” alitangaza Mbowe na kufanya uwanja kulipuka kwa shangwe.
Mbowe aliyeambatana na wabunge kadhaa
akiwamo Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini, alijinasibu kuibuka na
ushindi wa kishindo yeye na chama chake katika uchaguzi ujao kuanzia
jimbo la Hai na katika majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kama sheria ingekuwa inaruhusu
ningefurahi iwapo CCM ingesimamisha wagombea zaidi ya 10 katika Jimbo la
Hai ili wapambane na mimi kwa sababu mgombea mmoja pekee siyo saizi
yangu,” alijinasibu Mbowe.
Hukumu dhidi yake
Akizungumzia hukumu iliyomtia hatiani na
kuhukumiwa faini au kifungo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani
Bungeni alisema alikusudia kwenda jela kuwakilisha mamilioni ya
Watanzania wanaosota huko “kwa kesi na hukumu za kipuuzi”.
“Kama kesi ya mtu mwenye dhamana ya
uwakilishi wa wananchi kwa nafasi ya ubunge inaweza kuendeshwa kwa zaidi
ya miaka minne na hukumu kutolewa katika mazingira tatanishi kama
ilivyokuwa kwangu, Watanzania wa kawaida wanateseka kiasi gani?” alihoji
Mbowe.
Alidai kuwa baada ya kumhukumu kifungo
cha mwaka mmoja au faini ya Sh1,000,000, Hakimu Denis Mpelembwa
amepandishwa cheo kuwa hakimu mkazi na kuhamishiwa mkoani Kagera, siku
moja tu baada ya hukumu.
“Kilichokuwa
kinatafutwa ni namna ya kumzuia Mbowe asigombee ubunge Hai kwa sababu
CCM wanajua nguvu yangu. Wamekosea sana kwa sababu hukumu ile hainizuii
kugombea. Nitaombea na nitashinda kwa kishindo,” alisema.
0 comments:
Chapisha Maoni