HATUA
ya wanawake wengi kuchelewa kwenda hospitali kwa wakati pindi
wanapokuwa wajawazito, imewafanya 140 kufariki kwa mwaka katika Mkoa wa
Mwanza kwa uzazi huku 53 kati yao wakitoka katika Wilaya ya Sengerema
mkoani hapa.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Ismael
Sarumbo, wakati wa uzinduzi wa chumba cha upasuaji na wodi ya wazazi
katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.
Alisema katika wilaya za Mkoa wa Mwanza, Sengerema inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na uzazi.
“Sehemu
kubwa ya wilaya hii ni eneo la visiwa hivyo kuchelewa kuhudhuria
kliniki wakati wa ujauzito kwa wanawake bado ni changamoto ambayo
tunakabiliana nayo,” alisema Dk. Sarumbo.
Kwa
upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Sengerema, Dk.
Marie Jose, alisema hospitali ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la akina
mama wengi kupoteza maisha kutokana na kuwa na miundombinu isiyokidhi
viwango, ambapo wagonjwa watatu walikuwa wakitumia kitanda kimoja.
Naye
msimamizi wa hospitali hiyo, Joseph Massawe, alisema hospitali hiyo kwa
sasa inakabiliwa na tatizo la madaktari na wameiomba Serikali kuangalia
namna ya kutatua tatizo hilo.
Mmoja
wa akina mama wanaotumia wodi hiyo, Catherine Deus, ameushukuru uongozi
wa hospitali kwa hatua hiyo ya kuongeza wodi za wazazi na kusema
itasaidia kupunguza tatizo lililokuwepo awali la wanawake watatu
kutumia kitanda kimoja.
0 comments:
Chapisha Maoni