test

Jumatatu, 18 Mei 2015

Njaa yabisha hodi Wilaya ya Chamwino




WANAWAKE wa Kijiji cha Suli Kata ya Fufu wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wameiomba Serikali iwape msaada wa chakula cha dharura kutokana na kukabiliwa na baa la njaa wilayani humo.
 
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wameanza kwenda maporini kutafuta ubuyu kwa ajili ya chakula.
 
Wakizungumza kijijini hapo kwa nyakati tofauti, walisema hivi sasa hali imekuwa mbaya kwao na wanashindwa kujua la kufanya.
 
Akizungumza mmoja wa wananchi hao,  Imani Ezekel, alisema kuwa katika kijiji hicho kuna hali mbaya ya uhaba wa chakula hali ambayo inawalazimu kwenda maporini kutafuta ubuyu kwa ajili ya chakula.
 
“Wanawake na watoto ndio tunaohadhirika sana na tatizo hili la njaa baada ya wanaume wetu wakiwemo hata vijana wa hapa vijijini kukimbilia huko bwawani kwa lengo la kutafuta vibarua ili waweze kupata fedha za kununulia chakula,” alisema Imani.
 
Naye Doris Mnyeule, alisema kutokana na hali ya ukosefu wa chakula katika kijiji hicho, wanalazimika kutumia muda mwingi kwenye miti ya ubuyu na ukwaju wakiwemo na watoto wao ili waweze kupata hata wa kutengeneza uji kwa ajili ya familia zao.
 
“Muda mwingi wanatumia kutafuta ubuyu na ukwaju ili waweze kupata wa kutengeneza uji kwa ajili ya familia, huku wakati mwingine tukitumia wakati huo kutafuta vibarua vya kulima,” alisema.
 
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji, Cilem Masinga, alikiri kuwepo kwa njaa kwa wananchi wake na kuiomba Serikali kupeleka chakula cha bei nafuu ili waweze kukinunua.
 
Alisema hivi sasa baadhi ya wanaume wamezikimbia familia zao kwa lango la kwenda kutafuta vibarua kwenye bwawa la Mtera huku wengine wakitumia wakati mwingi maporini kutafuta ubuyu na ukwaju.
 
“Ni kweli hali ya chakula siyo mzuri hapa kijijini kwangu kutokana na hivi sasa walio wengi wanategemea chakula cha ubuyu na ukwaju kutokana na mwaka huu kutokunyesha mvua za kutosha kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” asema Masinga.
 
Akitoa ufafanuzi kuhusu hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Farida Mgomi, alisema hali hiyo ya kuwepo kwa njaa katika maeneo mengi ya vijiji vya wilaya hiyo pamoja na mkoa mzima kwa ujumla, inatokana na ukame wa mvua zilizonyesha mwaka huu na kusababisha kukosekana kwa chakula cha kutosha.
 
“Kwa ujumla kwa mwaka huu katika mkoa wetu wa Dodoma hali ya mvua haikuwa mzuri, hali ambayo imeleta tishio la ukosefu wa chakula ikiwemo na njaa kwa wananchi walio wengi huko vijijini, lakini hata hivyo Serikali itahakikisha inapeleka chakula cha bei nafuu kwa haraka ili wananchi waweze kununua,” alisema.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni